2015-10-31 09:02:00

Mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu ni dhamana ya kimaadili


Baba Mtakatifu Francisko anasema mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu ni dhamana endelevu ya kimaadili miongoni mwa viongozi wa  Kanisa na Serikali kwani biashara hii ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Huu ni ujumbe ambao Baba Mtakatifu amewatumia viongozi wa Kanisa, Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama wanaounda Kikundi cha Mtakatifu Martha katika mkutano wao ulioanza hapo tarehe 30 hadi 31 Oktoba 2015 huko, Madrid, Hispania.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi hawa kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya binadamu inatokomezwa kutoka katika sura ya nchi, kwa kuwakomboa watu kutoka katika utumwa mamboleo. Haya ni mambo yanayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Wahusika wa biashara hii watiwe mbaroni na mkondo wa sheria ufanye kazi yake. Iwe ni fursa ya kuwafichua wale wote wanaojihusisha na biashara ya binadamu pamoja na kuendelea kuwasaidia waathirika, ili kuanza tena upya historia ya maisha yao kwa kuwa na matumaini mapya.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wito wake katika mapambano  dhidi ya biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo ni mambo ambayo yamepambanuliwa kwa kina na mapana katika ajenda ya maendeleo ifikapo mwaka 2030 pamoja na kufuta kazi za suluba wanazofanyishwa watoto wadogo, ikiwa ni pamoja na kupelekwa mstari wa mbele katika mapambano ifikapo mwaka 2025. Haya ni mambo ambayo yanahitaji kuwekewa sera na mikakati inayotekelezeka, sanjari na utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote.

Ubaguzi wa kijamii na kiuchumi ni kurasa chungu ambazo zinaendelea kusababisha madhara makubwa kwa ustawi na maendeleo ya wengi anasema Baba Mtakatifu. Hili ndilo chimbuko pia la biashara haramu ya viungo vya binadamu inayoendelea kushamiri kama mtende wa Lebanon. Bado kuna biashara haramu ya dawa za kulevya, utalii wa ngono, ukahaba, biashara ya silaha na vitendo vya kigaidi mambo ambayo kimsingi yanahatarisha utu na heshima ya binadamu. Ni jukumu la viongozi pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, uhalifu dhidi ya binadamu unapatiwa kisogo kwa kushughulikiwa kikamilifu bila kuogopa wala kuwa na makunyanzi! Uwepo ushirikiano wa kudumu, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu, sanjari na kuhakikisha kwamba, uhuru, utu na heshima ya binadamu vinakuzwa na kudumishwa na wote.

Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake anakaza kusema, anaendelea kuwaombea ili utume huu uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, ili kuganga na kuponya madonda yanayoendelea kusababisha mateso kwa watu wasiokuwa na hatia; matendo ambayo yanaamsha pia Madonda ya Kristo. Biashara haramu ya binadamu inapaswa kuvaliwa njuga hadi kieleweke, kwani mapambano haya yanapania kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Itakumbukwa kwamba, Kikundi cha Mtakatifu Martha, kilianzishwa kunako mwaka 2014 na kinaongozwa na Kardinali Vicent Gerald Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles pamoja na Bwana Bernard Hogan-Howe, Kamanda wa Polisi wa Jiji la London, Uingereza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.