2015-10-30 08:05:00

Umoja wa Ulaya unapaswa kushikamana kukabiliana na changamoto ya wakimbizi


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 29 Oktoba 2015 amekutana na kuzungumza na Bibi Dalia Grybauskaitè, Rais wa Jamhuri ya Wananchi wa Lithuania ambaye baadaye amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Vatican wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya viongozi hawa, wameshukuru kwa namna ya pekee mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Lithuania. Wamegusia pia masuala yanayogusa mambo ya kikanda pamoja na umuhimu wa kudumisha mshikamano Barani Ulaya ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza kama vile: wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi ya maisha Barani Ulaya; amani na usalama kikanda na kimataifa; mgogoro wa Ukraine pamoja na hali tete iliyoko huko Mashariki ya Kati, hususan Syria na Nchi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.