2015-10-30 08:16:00

Majadiliano ya kidini ni msingi wa maridhiano na fursa ya watu kukutana!


Kanisa Katoliki linapojikita katika majadiliano ya kidini linapenda kutambua na kuthamini yote yaliyo kweli na matakatifu katika dini mbali mbali duniani. Linaheshimu sheria na mafundisho ya dini hizi, ili kukuza na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa mataifa, tayari kila waamini kuweza kutolea ushuhuda wa imani ya dini zao. Lengo ni kudumisha mema ya maisha ya kiroho, kimaadili pamoja na tunu msingi za kijamii na kitamaduni kutoka kwa waamini wa dini mbali mbali.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, Alhamisi tarehe 29 Oktoba 2015 wakati akishiriki kwenye Kongamano la kimataifa la majadiliano ya kidini huko Moroco lililoandaliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Majadiliano ya kidini na Kitamaduni wa Ducci, Fes, nchini Morocco. Kongamano hili limeongozwa na kauli mbiu “Majadiliano ya kidini ni msingi wa maridhiano na fursa ya watu kukutana”. Huu ni mwendelezo wa makongamano ya kimataifa kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani, yaani "Nostra Aetate".

Kanisa Katoliki linajikita katika majadiliano ya kidini kwa kutambua kwamba, nyakati hizi kuna mwingiliano mkubwa wa watu, ambao kimsingi asili na hatima ya maisha yao ni moja. Kama binadamu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wanaendelea kujiuliza maswali ya msingi kuhusu: binadamu, maisha, wema na dhambi; njia ya  kuweza kujipatia furaha ya kweli, mauti na uzima wa milele. Haya ni mambo msingi yanayoweza kuimarisha na kudumisha umoja, udugu na mshikamano kati ya watu, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Abrahamu, Baba wa imani.

Kardinali Sandri anakaza kusema, kwa kutambua na kuheshimu mafundisho makuu ya kidini, waamini wanaweza kujikita katika mchakato wa kudumisha haki, amani, upendo, maridhiano na mafao ya wengi, binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Majadiliano ya kidini ni fursa makini kwa waamini wa dini mbali mbali kufahamiana, kuheshimiana na kuepuka misimamo mikali ya kidini ambayo katika kipindi cha miaka michache iliyopita imekuwa ni chanzo cha kinzani, mipasuko ya kijamii na maafa makubwa kwa watu na mali zao. Waamini wafahamu fika mafundisho ya dini zao, tayari kuyatolea ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Lengo ni kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu na kujieleza pamoja na kujenga tunu msingi za maisha ya kiutu, kitamaduni na kijamii, ili waamini wawe kweli ni vyombo vya haki, amani na upendo na madaraja ya watu kukutana na kusaidiana badala ya kutoa nafasi kwa wahubiri wenye misimamo mikali ya kidini kuchafua mahusiano ya watu kwa misingi ya udini. Viongozi wa Serikali mbali mbali wahakikishe kwamba, uhuru wa kuabudu unalindwa na kudumishwa kwa ajili ya mafao ya wengi. Lakini kwa bahati mbaya, leo hii kuna Serikali ambazo zinaendelea kukandamiza uhuru wa kuabudu kama alivyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anazungumzia kuhusu uhuru wa kidini huko Philadelphia Marekani. Dini liwe ni jukwaa na msingi wa haki, maridhiano, heshima, utu na haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.