2015-10-30 14:10:00

Kumbu kumbu ya miaka 40 ya Uhuru wa Angola ikuze maridhiano!


Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tomè  na Principe, CEAST, linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho ya miaka 40 tangu Angola ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Wareno, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mchakato wa umoja na upatanisho wa kitaifa. Maaskofu wanatarajia kufanya mkutano wao wa mwaka kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 10 Novemba 2015 na baada ya mkutano huu wanatarajiwa kutoa barua ya kichungaji.

Maadhimisho ya Miaka 40 ya uhuru wa Angola ni tukio muhimu sana katika maisha ya wananchi, itakuwa ni fursa ya kufanya upembuzi yakinifu kwa kuangalia walikotoka, mahali walipo na matarajio ya wananchi wa Angola kwa siku za usoni! Haya ni mambo yatakayofanyiwa kazi kwenye kongamano la kimataifa lililoitishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Angola.

Haki, amani na upatanisho ni mambo makuu yanayoendelea kufanyiwa kazi na Maaskofu wa Angola wakati huu wanapoadhimisha Mwaka wa Ekaristi Takatifu uliozinduliwa Mwezi Mei, 2015 na unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 21 Agosti 2016. Maaskofu wanaendelea kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuangalia kwa kina na mapana mchango na utume wa Kanisa Katoliki nchini Angola. Ni kipindi muafaka cha kutafakari kwa kina historia ya Angola ambayo kimsingi inakumbatia kurasa chungu za vita na kinzani mambo ambayo yameacha madonda makubwa kwa wananchi wengi wa Angola. Umefika wakati wa kumwilisha haki, amani na upatanisho, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.