2015-10-29 15:20:00

Waamini iweni mashuhuda wa majadiliano ya kidini katika ukweli, uwazi na haki


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Oktoba 2015 anafanya hija ya kichungaji nchini Morocco pamoja na mambo mengine anashiriki katika kongamano la kimataifa la majadiliano ya kidini muhimu sana katika mchakato wa watu kukabiliana na changamoto za maisha, tayari kujikita katika majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi. Akiwa nchini Morocco amewatembelea na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Kanisa pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Mtakatifu Francisko iliyoko Fez.

Katika mahubiri yake amewashukuru waamini wa Parokia ya Mtakatifu Francisko kwa kusimama imara katika imani, licha ya uchache wao katika eneo hili ambalo linakaliwa na idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam. Wanatambua kwamba, wao ni sehemu ya familia na wateule wa Mungu, ambao imani yao imesimikwa kwenye msingi wa Mitume wa Yesu na Kristo ndiye kiongozi mkuu. Anasema waamini wanapaswa kutambua kwamba, familia ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, dhana ambayo imepembuliwa kwa kina na mapana na Mababa wa Sinodi ya familia, iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Familia zijenge utamaduni wa kushiriki mara kwa mara Mafumbo ya Kanisa pamoja na kusikiliza Neno la Mungu linalopaswa kuwa ni dira na taa inayoyaongoza maisha yao. Waamini wajenge utamaduni wa kusali kama njia ya kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao ya kiroho. Sala imwilishwe katika huduma ya matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji. Waamini wawe tayari kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha yao, daima wakionesha upendo kwa Mungu na jirani.

Kardinali Sandri anawataka waamini nchini Morocco kuwa na imani thabiti inayojikita katika Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na matakatifu pamoja na sala, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika haki, amani, upendo na mshikamano. Hii ni changamoto ya kutubu na kuendelea kumwongokea Mungu kila siku ya maisha. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Kardinali Sandri amewasilisha pia salam na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.