2015-10-29 08:11:00

Mshikamano na wananchi wa Pakistan na Afghanstan waliokumbwa na maafa!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake  Jumatano, tarehe 28 Oktoba 2015, amewakumbuka na kuwaombea kwa namna ya pekee kabisa wananchi wa Pakistan na Afghanstan waliokumbwa na tetemeko la ardhi ambalo limesababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Baba Mtakatifu amewaombea marehemu wote ili waweze kuona mwanga wa milele; majeruhi waweze kupona na kurejea tena kuendelea na shughuli zao; watu wasiokuwa na makazi, wapate msaada; na kwamba, wote hawa waguswe na huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; waendelee kuwa wajasiri na watu wote wenye mapenzi mema wawaoneshe mshikamano wa upendo.

Wakati huu Mama Kanisa anapohitimisha Mwezi wa Rozari Takatifu, anawaalika waamini kwa namna ya pekee, kukuza na kudumisha Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili katika maisha yao. Tarehe 28 Oktoba ya kila mwaka, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Watakatifu Simoni na Yuda mashuhuda wa Injili. Baba Mtakatifu anawaomba mashuhuda hawa wasaidie kukuza imani na kuimarisha mapendo miongoni mwa wafuasi wa Kristo, kama kielelezo cha imani tendaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.