2015-10-29 08:22:00

Majadiliano ya kidini ni changamoto endelevu ili kujenga amani, upendo na udugu


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Vatican walisoma alama za nyakati kwa kuona mabadiliko ya kasi yaliyokuwa yanaendelea kujitokeza ulimwenguni na kuamua kuanza mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kujenga na kuimarisha: umoja, udugu na urafiki kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Familia ya Mungu inamshukuru kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamua kufanya kumbu kumbu ya Jubilei hii kwa kutoa katekesi maalum juu ya Tamko la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Vatican kuhusu majadiliano ya kidini, Nostra Aetate, Jumatano tarehe 28 Oktoba 2015.

Kardinali Jean Lous Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini ameyasema haya kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambulisha wajumbe waliokuwa wanashiriki katika Kongamano la kimataifa la maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya majadiliano ya kidini pamoja na wawakilishi kutoka katika dini mbali mbali, kielelezo makini kwamba, waamini wa dini mbali mbali wanaweza kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kardinali Tauran anakaza kusema, majadiliano ya kidini ni muhimu sana, lakini katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita kumekuwepo na changamoto kubwa. Kanisa linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuhimiza majadiliano ya kidini, ili kuwawezesha watu kukutana, huku wakiheshimiana, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, haki, amani na mapendo. Waamini wanaweza kulifanikisha kwa kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu, ukosefu wa usawa pamoja na kutunza mazingira, nyumba ya wote. Sala ya kuombea amani iliyoadhimishwa mjini Assisi ni kielelezo kwamba, mshikamano na udugu kati ya waamini wa dini mbali mbali ni jambo linalowezekana kabisa!

Naye Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo, katika maadhimisho haya, amewatambulisha wajumbe wa Jumuiya ya Wayahudi Duniani waliokuwa wanashiriki katika Kongamano la kimataifa la maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Nostra Aetate. Lengo ni kuendeleza utamaduni wa watu kukutana, dhana inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake.

Cheche za majadiliano na waamini wa dini ya Kiyahudi ziliibuliwa kunako mwaka 1960 wakati ule Mtakatifu Yohane wa XXIII alipokutana na kuzungumza na Bwana Jules Isaak. Tangu wakati huo, mchakato wa majadiliano na waamini wa dini ya Kiyahudi ukaanza kushika kasi na matunda yake yakatolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao la Nostra Aetate, walioonesha amana ya maisha ya kiroho kati ya Wakristo na Wayahudi kadiri ya Maandiko Matakatifu. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakalaani vitendo vyote vinavyonyanyasa na kuwadhulumu waamini wa dini mbali mbali. Tangu wakati huo, Kanisa limeendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini kama hata ambavyo inajionesha kwa Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Nchi Takatifu akaenda kusali kwenye Ukuta wa machozi pamoja na kutembelea kwenye Makumbusho ya Yad Vashem.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.