2015-10-29 09:34:00

Kardinali Pengo: Msiwaruhusu wanasiasa kuvuruga amani kwa misingi ya udini!


Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipopitisha Tamko kuhusu majadiliano ya kidini linalojulikana kwa lugha ya Kilatini kama “Nostra Aetate”. Lengo ni kujenga na kudumisha: haki, umoja, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa mataifa, tayari kujikita katika kutafuta mafao ya wengi na maendeleo endelevu ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Tofauti za kidini zinapaswa kuwa ni kielelezo cha utajiri wa watu na kamwe zisiwe ni sababu na chanzo cha kinzani na mpasuko wa kijamii.

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Radio Vatican hivi karibuni alikaza kusema, vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za Bara la Afrika vinapata chimbuko lake katika misimamo mikali ya kidini inayochochewa na baadhi ya watu ndani ya jamii kwa ajili ya mafao yao binafsi. Hawa ni watu wanaotaka kuona Jamii inameguka kutokana na machafuko ya kidini, ili waweze kujiimarisha kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata wakati mwingine kidini, jambo ambalo ni hatari kubwa sana kwa mafungamano ya kijamii.

Kardinali Pengo anasema, kuna haja kwa waamini wa dini mbali mbali, lakini kwa namna ya pekee Barani Afrika  kwa Wakristo na Waislam kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; tayari kupokea na kuheshimu tofauti zao za kidini, ili kuimarisha haki msingi za binadamu, amani, utulivu na maendeleo ya wengi. Watu wanaochochea vitendo vya kigaidi na malumbano ya kidini ni watu wenye kutafuta mafao yao binafsi na kamwe wasingependa kuona jamii inajikita katika misingi ya haki, amani na utulivu.

Watu wa namna hii hawaweze kupokea ukweli halisi, bali wanataka kujinufaisha kwa kutumia tofauti za kidini ili kuwajengea watu jazba na hasira, ili wao waweze kufaidika. Ni wajibu wa waamini wenyewe kukataa kishawishi cha kutumbukizwa katika malumbano, kinzani na machafuko ya kidini kwa kusimamia ukweli, maadili na utu wema. Serikali ziwe mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, uhuru wa mtu kujieleza pamoja na kudumisha amani na utulivu, mambo msingi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Majadiliano ya kidini yajisimike katika ukweli, uwazi na ustawi wa wengi; tayari kuanzisha mchakato wa kusaidiana na kuhudumiana kwa ajili ya mafao ya wengi. Misimamo mikali ya kidini ni hatari sana kwa mafungamano ya kijamii na kamwe wanasiasa wasiruhusiwe kugeuza uwanja wa kidini kuwa uwanja wa mapambano kwa ajili ya mafao yao binafsi. Dini ni chombo cha kukuza na kudumisha utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano kati ya jamii ya watu na wala kisiwe ni chanzo cha mpasuko wa kijamii na malumbano yasiyokuwa na kita wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.