2015-10-28 10:44:00

Padre Luka, aliyewahi kuwa Msimamizi wa kitume Jimbo la S'wanga amefariki dunia


Mheshimiwa Pd. Walter Luekewille alizaliwa tarehe 1 Februari 1930 katika kijiji cha Verl – Ujerumani. Baada ya majiundo yote katika Shirika la Wamisionari wa Afrika na katika malezi ya kiseminari, tarehe. 26.05.1955 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mwaka 1959 alitumwa rasmi Tanzania - Sumbawanga kama Mmisionari. Alifanya kazi katika Parokia za Chiwanda (wakati ule 1959-1962), Chala (1962-1971), Mamba (1971-1984) na Sumbwanga (1984-2002); Mwaka 2002 – 2004, alifanya kazi katika Jimbo la Mpanda.

Pamoja na mambo mengine mengi aliyowahi kutenda kama Padre, mtawa na mmisionari mtiifu, ni kwamba: mwaka 1994 baada ya kifo cha Mhashamu Askofu Kaloro Msakila, Pd. Walter Luekewille aliteuliwa na Vatican kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Sumbawanga. Aliifanya kazi hiyo kwa uaminifu kwa muda wa miaka mitatu hadi pale alipoteuliwa Askofu Damian Kyaruzi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga.

Kuanzia mwaka 2002-2004 alisaidia katika kulijenga Jimbo Jipya la Mpanda. Na mwaka 2004 kwa maamuzi ya Wakubwa wa Shirika na kwa vifungo vya utii, alirudi Ujerumani katika Nyumba ya Wamisionari wa Afrika (Afrikanum) iliyoko mjini Koloni. Hapo aliendelea kutoa huduma za kiroho kwa jumuiya na kwa waamini. Januari mwaka 2014, alihamishiwa katika nyumba ya wazee huko Trier, ambako aliishi pamoja na wazee wengine wengi waliofanya kazi ya Umisionari katika maeneo mbalimbali ya Afrika. Hata hapo pia aliendelea kutoa huduma mbalimbali za kiroho, akiwa mwenye afya, nguvu na furaha tele.

Mwezi Mei 2015 Mheshimiwa sana Pd. Walter Luekewille, aliadhimisha Jubilei ya Miaka 60 ya Upadre. Siku chache baadaye ghafla alipata shida ya afya na akagundulika kuwa ana Saratani ya ini. Ugonjwa huo ulimletea udhaifu mkubwa wa mwili kwa kipindi cha miezi mitano tu, na tarehe 17.10.2015, saa 04:45, mwenyezi Mungu alimwita kwake kuhani wetu, mmisionari wetu na mpendwa wetu Pd. Walter Luekewille M.Afr. Ameuhama ulimwengu huu akiwa tayari kwenda kwa Baba wa milele, na ameitoa pumzi yake ya mwisho akiwa mwenye imani thabiti na ufahamu. Muuguzi anasema, dakika za mwisho alitamka ‘sasa ninakwenda’ na kwa uso wa tabasamu akatoa pumzi yake ya mwisho! Hakika, amevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo ameumaliza na imani ameilinda!

Tar. 23.10.2015, Hayati Padre Walter Luekewille M.Afr, amelazwa katika nyumba ya mwisho pamoja na wamisionari wengine huko Trier – Ujerumani. Ibada ya Maziko ilihudhiriwa na umati mkubwa wa Wamisionari wa Afrika wake kwa waume, ndugu, jamaa, marafiki, pamoja na wawakilishi wachache kutoka Jimbo la  Sumbawanga ambako alifanya kazi takribani miaka 50 ya uhai wake.

Katika misa ya Maziko iliyoongozwa na Mkuu wa Provinsi ya Ujerumani; mhubiri katika misa hiyo ambaye ni Pd. Zepp Hochheimer mkuu wa nyumba ya Wazee Trier, alimwelezea Hayati Pd. Walter Luekewille kuwa alikuwa mtu wa kiroho aliyependa maisha ya sala, tafakari na ari ya kimisionari yenye kulenga kumkomboa mtu kiroho na kimwili. Ndiyo maana sehemu zote alizoishi, alijihusisha si tu katika kuhubiri imani, bali alijibidisha kwa dhati katika kutoka huduma za kijamii kwa watu wote, kielelezo cha Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Mhubiri huyo aliendelea kusema, katika maisha na utumishi wake, mheshimiwa sana Pd. Luka aliongozwa na Injili ile ya safari ya Wanafunzi wa Emaus (Lk. 24:35), ambapo Kristo Bwana aliambatana nao na aliwapa Katekesi juu ya utume wa Mkombozi na mwishoni Kristo mwenyewe anajidhihirisha kwao katika kuumega mkate. Baada ya hapo wanapata nguvu, giza linaondoka, wanasindikizwa kwa nguvu ileile, na wanafanywa kuwa mitume kwa mitume. Kwa ujasiri wale wanafunzi wa Emaus wanarudi Yerusalemu kuwapasha habari wanafunzi wengine kuwa Kristo amefufuka kweli. Na huu ndio ulikuwa msukumo mkubwa kwa Pd. Walter Luekewille kuwa tayari kuambatana na watu na kuwahubiria  habari njema ya Kristo.

Ni katika msingi huo alisema Pd. Hochheimer, Pd. Walter Luekewille katika utumishi wake kama kuhani na kwa namna ya pekee alipofanywa kuwa msimamizi wa Kitume kwa Jimbo la Sumbawanga, alikazia sana umuhimu wa Katekesi kwa Waamini; ndiyo maana akaahimiza uwepo wa vikundi vya utume wa Kibiblia, Karismatiki na vikundi mbalimbali vya Sala. Aliamini kwamba kwa njia ya Neno la Mungu na Katekesi makini, waamini wanajaliwa kuufahamu undani wa imani tayari kumsadiki, kumwambata na kumshuhudia Kristo Yesu

Ili kuimwilisha Injili ya Kristo, akisaidiwa kwa kiasi kikubwa sana na ndugu zake na Jimbo lake la Paderbon, aliweza kujenga makanisa ya Kristo Mfalme, Familia Takatifu, Roho Mtakatifu, Hospitali ya Kristo Mfalme, Duka la Vitabu la Jimbo, Shule mbalimbali, Kituo cha Kiroho cha Mtakatifu Libori, barabara pamoja na huduma za maji. Hakika, alilenga kumkomboa mwanadamu kimwili na kiroho.

Wakati misa ya mazishi inaadhimishwa huko Trier Ujerumani, muda huohuo Jimboni Sumbawanga Misa Takatifu ya kumsindikiza Pd. Walter Luekewille ilikuwa ikiadhimishwa katika Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Sumbawanga. Askofu Damian Kyaruzi, Mapadre, Watawa na Waamini wasio na idadi kutoka katika Makanisa ambayo kwa namna ya pekee Hayati Padre Luka alihusika katika kuyajenga na kuyahudumia; walikusanyika pamoja na kuadhimisha sadaka ya Bwana ili kumwombea pumziko lenye heri.

Naye Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi wa Jimbo katoliki Sumbawanga  katika mahubiri yake, alimwelezea Pd. Walter Luekewille kama Baba aliyejawa na imani thabiti kwa Mungu hata akajitoa kikamilifu katika kumtumikia Mungu kwa kuihubiri Injili ya Kristo nyakati zote na katika mazingira ya aina zote.

Aliendelea kumweleze Pd. Luka kama mtu aliyekuwa na moyo wa upendo kwa watu wote bila ya ubaguzi, na ndiyo maana alijikita katika kutoa huduma za kimwili kwa watu wote, tena pasipo na ubinafsi. Na zaidi ya hayo nyakati zote, alitumia vipawa vyake vyote katika kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili. Askofu Damian Kyaruzi aliwaalika  waamini wote kuiga mfano wa waleta imani wetu¸ambao waliitangaza imani hiyo siyo kwa maneno tu, bali hata kwa mfano wa maisha yao, kwa jasho lao, kwa machozi yao na wengine kwa damu yao.

Ni maneno hayo hayo ndiyo yaliyofunga mahubiri ya Pd. Hochheimer kule Trier aliposema “Mpendwa Pd. Luka, Pd. Walter, tunatambua jinsi ambavyo Mungu wa pendo alikuinua nawe ukamtangaza. Umemtangaza Mungu wetu sio kwa maneno tu bali kwa maisha yako yote. Yeye mwenyewe awe pamoja nawe, akupe faraja ya maumivu yote, na awafariji wale wote ambao daima wamekuwapo pamoja nawe kwa kukujaalia amani na furaha ya milele”. Nasi Wanasumbawanga na Mpanda; pamoja na wanandugu wote, tunamwomba Mungu mwingi wa rehema, ampanguse jasho la kazi nzito Mmisionari wetu Pd. Walter Luekewille, ampe tuzo la haki, analostahili mtumishi mwema na mwaminifu; kwa kumshirikisha katika karamu ya wateule huko Mbinguni. Amina

Kukuletea taarifa hii kupitia Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB, kutoka Abasia ya Mvimwa – Sumbawanga.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.