2015-10-28 16:09:00

Miaka 50 ya mchakato wa majadiliano ya kidini uendeleze haki na amani!


Mwenyeheri Paulo VI, katika maisha na utume wake, alitoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na waamini wa dini mbali mbali duniani kama inavyojidhihirisha katika Tamko la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Nostra Aetate, ambalo Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu lilipotolewa. Papa Paulo VI alianzisha Sekretarieti kwa waamini wa dini mbali mbali, leo hii ni Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini.

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican lilikuwa ni tukio la neema iliyoliwezesha Kanisa  kusoma alama za nyakati kwa kujitafakari na kuangalia ulimwengu, ili liendelee kuwa aminifu kwa Mapokeo na historia ya watu wa nyakati hizi. Mwenyezi Mungu kwa nyakati mbali mbali amezungumza kwa njia ya Manabii na wakati wa utilimifu wa nyakati amezungumza kwa njia ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo.

Huu ni muhtasari wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 28 Oktoba 2015, Kanisa linapoadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu majadiliano ya kidini, Nostra Aetate, tukio ambalo limehudhuriwa na waamini kutoka katika dini mbali mbali, waliokusanyika mjini Vatican, ili kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, majadiliano ya kidini ni changamoto endelevu inayojikita katika uhalisia wa maisha ya watu kutokana na ukweli kwamba, kuna mwingiliano mkubwa wa watu wanaotegemeana; watu wanaendelea kujiuliza maswali ya msingi kuhusu: maana ya maisha, mateso na kifo; mwanzo na hatima ya maisha ya binadamu; umoja wa familia ya binadamu; dini na dhamana yake katika kumtafuta Mwenyezi Mungu anayepatikana kati ya watu, tamaduni na jamaa. Kanisa liyaangalia mambo ya kweli na matakatifu yanayopatikana kutoka katika dini nyingine na kuthamini: maisha ya kiroho na kanuni maadili.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia kwamba, Kanisa linapenda kudumisha majadiliano na waamini wa dini mbali mbali, lakini daima likiwa aminifu katika ukweli mfunuliwa kwamba, wokovu wa dunia unapatikana kwa njia ya Yesu Kristo na kwamba, Roho Mtakatifu ni chemchemi ya amani na upendo. Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, Kanisa limeshuhudia kukua na kuendelea kwa mchakato wa majadiliano ya kidini.

Wengi bado wanakumbuka mkutano wa kuombea amani ulioitishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1986, mjini Assisi na alipokuwa mjini Calablanca, aliwataka vijana wa Kiislam kujenga na kudumisha urafiki na umoja kati ya watu! Moto wa matumaini miongoni mwa watu uliwashwa mjini Assisi. Majadiliano ya kidini yameendelea kukuza na kuimarisha mahusiano mema na waamini wa dini ya Kiyahudi, kwa kutambua amana ya maisha ya kiroho inayowaunganisha Wayahudi na Wakristo.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wamelaani mateso, dhuluma na nyanyaso zinazoweza kufanywa dhidi ya waamini wa dini nyingine. Wakristo na Waislam wanamtambua Mzee Ibrahimu kuwa ni Baba wa imani; wanamheshimu Bikira Maria; wanasubiri Siku ya hukumu ya mwisho; waamini wa dini hizi mbili wanasali, kufunga na kutoa sadaka. Majadiliano ya kidini yanapaswa kusimikwa katika misingi ya ukweli na uwazi; haki msingi za binadamu na zawadi ya maisha; uhuru wa dhamiri, mawazo na Ibada na kwamba, waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kushirikiana kwa dhati kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kushirikiana kwa ajili ya kukuza na kudumisha amani; kupambana na baa la ujinga, umaskini na maradhi; kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kuzuia mauaji na kinzani za kidini. Waamini wanapaswa kusimama kidete kupambana na rushwa pamoja na ufisadi wa mali ya umma; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na kumtangazia mwanadamu Injili ya matumaini na kwamba, sala ni muhimu sana kwa maisha ya kila mwamini.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, misimamo mikali ya kidini na vitendo vya kigaidi ni mambo ambayo yamesababisha kinzani na maafa makubwa kwa watu na mali zao; jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, tunu msingi za maisha ya kiroho zinakuzwa na kuimarishwa; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini ili kuendeleza mbegu ya urafiki; kwa kushirikiana katika kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Waamini katika umoja wao wanaweza kujiwekea mikakati na miradi ya kupambana na majanga katika maisha ya mwanadamu, ili kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anahitimisha kateksi yake juu ya majadiliano ya kidini kwa kuonesha matumaini yake katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, kwamba, iwe ni fursa ya kuimarisha mshikamano na huduma ya upendo kwa wote wanaotafuta ukweli katika maisha yao, licha ya umaskini wao wa hali na kipato. Waamini wawe kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu. Ili kudumisha majadiliano ya kidini, waamini wanapaswa kwanza kabisa kusali ili kutekeleza mapenzi ya Mungu, huku wakiheshimiana kwani wote ni ndugu wamoja wanaounda familia kubwa ya binadamu inayopaswa kuishi katika umoja na utofauti wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.