2015-10-28 11:55:00

Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa kuadhimishwa Cebu, Ufilippini


Kunako tarehe 17 Juni 2012, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alitangaza kwamba, maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 24 Januari hadi tarehe 31 Januari, 2016, huko Cebu, nchini Ufilippini. Maadhimisho haya na yaongozwa na kauli mbiu “”Kristo ndani mwenu, matumaini ya utukufu”.

Huu ni ufafanuzi ambao umetolewa na Askofu mkuu Piero Marin, Rais wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu kimataifa, alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumanne, tarehe 27 Oktoba 2015. Tukio hili limehudhuriwa na Askofu mkuu Josè S. Palma pamoja na Padre Vittore Boccardi, mjumbe wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu kimataifa.

Maadhimisho ya kongamano la Ekaristi Takatifu kimataifa yanalenga kuwa ni changamoto kwa familia ya Mungu Barani Asia, ili kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, sanjari na kujikita katika mchakato wa kuhamasisha ari na mwamko wa kimissionari, tayari waamini kujitosa kimaso maso kwenda kutangaza na kushudia Injili ya furaha kati ya watu wa mataifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini liliomba maadhimisho haya yafanyike nchini mwao, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Uinjilishaji nchini humo, yaani kuanzia mwaka 1521 hadi mwaka 2021.

Maadhimisho haya ni changamoto kwa Wakatoliki kujikita katika Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu, tayari kuchuchumilia mwamko wa kimissionari unaoambata azma ya Uinjilishaji, ili kuitangazia familia ya Mungu Barani Asia, Injili ya matumaini, licha ya matatizo na changamoto inayokabiliana nazo anasema Askofu mkuu Josè S. Palma, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cebu. Katika miaka ya hivi karibuni, Bara la Asia limekuwa ni kikolezo kikuu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, lakini bado kuna watu wengi wanasubiri kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu na kwamba, pamoja na kuliendeleza Kanisa Katoliki ambalo hadi sasa bado lina waamini wachache, ikilinganishwa na waamini wa dini nyingine.

Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu kimataifa yanapania kuwa ni chachu ya mchakato wa Uinjilishaji Barani Asia anasema Padre Boccardi ambaye, kwa muhtasari ametoa historia ya maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi takatifu kimataifa, kuwa ni mchakato wa hija ya familia ya Mungu inayotaka kujipyaisha kwa kumwambata Yesu wa Ekaristi Takatifu. Waamini wanakumbushwa kwamba, Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.