2015-10-27 09:06:00

Kuzeni mchakato wa haki, amani, upatanisho na maridhiano!


Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Poland na Ujerumani, wanaadhimisha kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 tangu walipoanza mchakato wa upatanisho kwa kusamehe na kuombana msamaha, ili kwa pamoja kuweza kutembea kwa umoja na ushirikiano licha ya changamoto wanazoweza kukutana nazo. Maaskofu kwa kulikumbuka tukio hili muhimu lililotokea kunako mwaka 1965 wameamua kulikumbuka tukio hili, lililofuatiwa na tamko la pamoja lililotiwa mkwaju huko Cracovia, tarehe 21 Septemba 2005 na Kardinali Karl Lehmann na J. Mikalik, Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Ujerumani na Poland.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameandika barua ya kumshukuru Balozi wa Poland mjini Vatican kwa mwaliko katika kumbu kumbu ya Jubilei hii ambayo inarejesha kwa namna ya pekee kabisa, kumbu kumbu ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kujikita katika safari ya upatanisho, haki na amani; ngumu, lakini muhimu sana kama sehemu ya mchakato wa kuponya madonda ya nchi hizi mbili kutokana na vita kuu ya pili ya dunia.

Huu ni mfano wa kuigwa kwa nchi mbali mbali zinazoendelea kuogelea katika vita, chuki na kinzani za kijamii. Baba Mtakatifu anashukuru kwa maonesho ya tukio hili la kihistoria yanayoendelea mjini Vatican. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho haya yatawasaidia wengi kufahamu historia ya nchi zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.