2015-10-27 11:49:00

Jubilei ya miaka 50 ya Tamko la Majadiliano ya kidini!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka 50 iliyopita walitoa tamko kuhusu majadiliano ya kidini kwa watu wa nyakati hizi linalojulikana kama “Nostra Aetate” linalokazia pamoja na mambo mengine dhamana ya Kanisa katika kuhamasisha umoja na upendo kati ya watu wa mataifa; kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kusimama kidete kutangaza na kushuhudia pamoja utu na heshima ya binadamu. Kanisa Katoliki linatambua mambo ya kweli na matakatifu katika dini mbali mbali, lina heshimu na kuthamini namna yao ya kutenda na kuishi; sheria na mafundisho yao.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Kanisa litaendelea kutangaza kwamba Yesu Kristo ni njia, ukweli na uzima na ambaye ndani mwake mwanadamu anapata utimilifu wa maisha ya utauwa na upatanisho kati yake na Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; mafao ya wengi, haki, amani na mshikamano wa kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 28 Oktoba 2015 anatarajiwa katika Katekesi yake, kujikita katika majadiliano ya kidini kama sehemu ya maadhimisho ya Tamko la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na Majadiliano ya kidini. Itakuwa ni fursa muafaka kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na waamini kutoka katika dini mbali mbali wanaoshiriki katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, Baraza la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo, Tume ya Kipapa ya mahusiano na Wayahudi pamoja na Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian.

Hii itakuwa ni fursa makini ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matunda mengi yaliyokwisha kupatikana katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, tangu Kanisa lilipojikita katika majadiliano ya kidini. Kanisa linatambua kwamba, bado kuna changamoto nyingi na vikwazo vya kufanyiwa kazi, lakini hadi hapa linapenda kumshukuru Mungu.

Mwenyeheri Paulo VI, tarehe 28 Oktoba 1965 wakati akifunga maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican alikaza kusema, Mtaguso ni kielelezo cha Kanisa linalosali, Kanisa linalojadiliana, Kanisa linalokua na Kanisa linaloendelea kujijenga, ili kukoleza mchakato wa majadiliano ya upendo na walimwengu. Waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kusimama kidete ili kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao; kulinda na kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano; sanjari na kukuza uhuru wa kidini. Elimu ya dini na malezi, ni muhimu sana katika kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.