2015-10-26 14:54:00

Kanisa limempoteza kiongozi mahiri aliyetetea uhuru na demokrasia ya kweli


Kardinali Jàn Chryzostom Korec, Askofu wa Jimbo Katoliki Nitra, Jamhuri ya Slovakia amefariki dunia tarehe 24 Oktoba 2015 akiwa na umri wa miaka 91; kiongozi aliyesimama kidete kuonesha dhamana ya Kanisa Katoliki katika mapambano dhidi ya utawala wa Kikomunisti; kwa kutetea uhuru na demokrasia ya kweli. Marehemu Kardinali Chryzostom alizaliwa kunako tatehe 22 Januari 1924. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa hapo tarehe 1 Oktoba 1950. Tarehe 24 Agosti 1951, akiwa na umri wa miaka ishirini na saba, akapewa Daraja takatifu la Uaskofu, mafichoni, ili kuwahudumia Wakristo waliokuwa wanadhulumiwa na utawala wa Kikomunisti.

Akaendelea na maisha na utume wake wa shughuli za kichungaji huku akifanya kazi za suluba katika mazingira magumu kwa muda wa miaka tisa, lakini kunako mwaka 1960 akakamatwa na kuhukumiwa kwenda jela na kazi ngumu kwa muda wa miaka kumi na miwili kwa kosa la kusaliti nchi. Akiwa gerezani alibahatika kukutana na Mapadre mia mbili pamoja na Maaskofu sita. Kunako mwaka 1968 akaachiliwa huru na kwa mara ya kwanza akaweza kuadhimisha Ibada ya Fumbo la Ekaristi Takatifu hadharani, tukio ambalo liliacha alama ya kudumu katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu.

Kunako mwaka 1969 akapata nafasi ya kukutana na Papa Paulo VI na hapo akapewa hati zake za kuteuliwa kuwa Askofu, miaka kumi na nane baada ya kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa Nitra. Mambo hayakuishia hapa, kunako mwaka 1974 akakamatwa tena na kutupwa gerezani ambako alikaa hadi mwaka 1984. Akiwa mafichoni, Askofu Jàn Chryzostom Korec alitoa Daraja takatifu la Upadre kwa Mapadre mia moja na ishirini. Kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka 1993 alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Slovachia. Kunako mwaka 1991 akateuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Kardinali. Ni mwandishi mahiri wa vitabu ambavyo vinaendelea kusomwa na watu wengi duniani.

Kwa kifo cha Kardinali Jàn Chryzostom Korec, Idadi ya Makardinali kwa sasa inakuwa ni Makardinali 218, kati yao Makardinali 118 wanahaki ya kupiga na kupigiwa kura na Makardinali 100 waliosalia hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura kadiri ya Sheria za Kanisa wakat iwa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.