2015-10-26 07:53:00

Hati elekezi kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya familia!


Mababa wa Sinodi ya familia katika hati yao elekezi mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya familia yaliyokuwa yanaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo”, wamesoma hati yao mbele ya Baba Mtakatifu Francisko. Hati hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Sura ya kwanza inaonesha jinsi ambavyo Kanisa linasikiliza familia: kiutu, kijamii na kiuchumi pamoja na kukazia umuhimu wa familia kushirikishwa katika sera na mikakati ya kijamii. Mababa wa Sinodi wanapembua kwa kina na mapana kuhusu familia, mahusiano na mafungamano ya kijamii pamoja na zawadi ya maisha.

Sura ya pili inajikita katika familia kadiri ya mpango wa Mungu. Hapa Mababa wa Sinodi wanaangalia familia minatarafu historia ya wokovu; familia kadiri ya mafundisho ya Mababa wa Kanisa, mafundisho tanzu na uelewa wa Kanisa kuhusu familia. Hapa Mababa wa Sinodi wanaangalia kwa kina na mapana mchango uliotolewa na Mababa wa Kanisa na Mapapa katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita.

Sura ya tatu inajikita kwa namna ya pekee katika utume wa familia unaoambata malezi ya kifamilia; familia, uzazi na umuhimu wa wazazi na walezi kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kutambua kwamba, wao ndio makatekista wa kwanza wa imani, maadili na utu wema; mambo wanayopaswa kuwarithisha watoto wao. Mababa wa Sinodi wanaangalia kwa kina na mapana mikakati ya shughuli za kichungaji inayopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kuhusu familia kwa kutambua kwamba, familia ni kitovu cha Uinjilishaji mpya. Mababa wa Sinodi wanakunja jamvi la hati yao kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa sala ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kusikiliza yote haya kwa makini, ameamuru hati hii ichapishwe ili familia ya Mungu iweze kuangalia, kutafakari na kumwilisha hayo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na Mababa wa Sinodi kama sehemu ya mchakato wa kutangaza Injili ya familia. Baada ya kila kipengele kusomwa, kikapigiwa kura ya siri na kupitishwa na Mababa wa Sinodi kwa asilimia kubwa. Familia ni mwanga katika giza la ulimwengu, ndiyo kauli mbiu inayoongoza yaliyomo kwenye hati ya mwisho ya Mababa wa Sinodi ya familia. Mababa wa Sinodi wamezingatia: Sheria na Nidhamu ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa.

Padre Federico Lombardi anafafanua kwamba, Mababa wa Sinodi wamefikia uamuzi wa kutoa kipaumbele cha pekee kwa familia zinazokumbana na mtikisiko wa imani, kwa kuzisikiliza na kuzisindikiza katika ukweli na uwazi; upendo na huruma ya Mungu. Hati nii ina utajiri mkubwa ikilinganishwa na hati nyingine zilizotangulia maadhimisho ya Sinodi ya familia na kwamba, mageuzi yaliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Ndoa zenye kinzani yamesaidia kwa kiasi kikubwa mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya familia.

Mababa wa Sinodi wamekazia kuhusu Mafundisho tanzu ya Ndoa na familia; ndoa ambayo inajikita katika upendo wa bwana na bibi, kwa kuonesha upendo wa Kristo kwa mchumba wake Kanisa. Huu ni ukweli mfunuliwa unaoonesha zawadi ya Mungu kwa binadamu. Ukweli na huruma ni sehemu na vinasaba vya maisha na utume wa Yesu kwa waja wake, mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa na Kanisa katika utekelezaji wa utume wa familia. Ndoa ni maadhimisho ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambaya  neema, huruma na upendo wa Mungu, ili kufikia ukamilifu wa ndoa na familia katika mwanga wa Injili.

Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, watu wenye mielekeo ya ushoga na ndoa za watu wa jinsia moja, wasitengwe wala kubaguliwa; wala Kanisa halitaweza kukubali kushinikizwa kutoka ndani wala nje ya Kanisa kukubaliana na mielekeo hii tenge katika maisha ya ndoa na familia. Mababa wa Sinodi wanawaangalia wakimbizi na wahamiaji kwa jicho la huruma na mapendo; wanaungana na familia zinazoteseka na kunyanyasika kutokana na vita na dhuluma za kidini; familia tenge bila kuwasahau watu wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu, viungo na utumwa mamboleo. Wote hawa waonjeshwe upendo na ukarimu wa Kanisa; wapokelewe na kupewa haki zao msingi.

Mababa wa Sinodi wanaendelea kukazia kwamba: maisha, utu na heshima ya binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza; kwa kuthamini dhamana na wajibu wa kila mtu katika familia. Wanawake wapewe nafasi ya pekee hata katika majiundo ya Wakleri; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi wasaidiwe na kwamba, familia zijenge na kuimarisha umoja na mshikamano wa dhati sanjari na kuepuka utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Familia ziwe ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo na kwamba, hata waamini ambao hawajafunga ndoa wanawajibika barabara katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Mababa wa Sinodi wanafafanua kwa masikitiko makubwa kwamba, misimamo mikali ya kidini, ubinafsi, umaskini, ukosefu wa fursa za ajira ni kati ya mambo yanayoendelea kutikisa misingi ya maisha ya ndoa na familia sehemu mbali mbali za dunia. Hali hizi zimeendelea kugumisha maisha ya familia kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na utume wake ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo.

Familia zihusishwe kikamilifu katika sekta ya elimu, utamaduni na kamwe, ubinafsi, utajiri na mali visiwe ndicho kiini cha mikakati ya kijamii na kiuchumi, bali utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu kwa kusimama kidete kupinga mambo yote yanayomdhalilisha binadamu! Familia zikumbatie Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Mababa wa Sinodi wanalitaka Kanisa kukuza na kudumisha malezi na majiundo kwa wanandoa watarajiwa, kwa kukazia usafi na sadaka kati ya wanandoa, ili kuweza kupokea zawadi ya watoto huku wakiwajibika kuwalea na kuwarithisha imani na tunu njema kutoka kwa wazazi wao. Watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu wanapaswa kupendwa na kuendelezwa na kwamba, wazazi ni Makatekista wa kwanza kwa watoto wao.

Wazazi walinde Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Sera za utoaji mimba na kifo laini ni matatizo yanayotishia ustawi na maendeleo ya familia. Familia ziendelee kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu; sanjari na kudumisha uhuru wa kidini.

Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, Kanisa linapaswa kusoma alama za nyakati kwa kuwa na matumizi ya lugha inayoeleweka na wengi katika mafundisho yake, kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika uhalisia wa maisha ya waamini. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, msingi wa maisha ya kijamii, kumbe, ni dhamana na jukumu la Kanisa na jamii katika ujumla wake kuhakikisha kwamba, ekolojia ya familia inadumishwa hata na viongozi wa kiserikali na kisiasa.

Mababa wa Sinodi wanahitimisha hati yao ya mwisho kwa kusema, huu ni mwanzo wa safari ya familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu akiona inafaa kwa kuzingatia ushauri na maoni yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi anaweza kuandika Waraka wa kitume utakaoendeleza dhana ya familia kadiri anavyoona inafaa. Mababa wa Sinodi wanasema, safari bado inaendelea hadi kieleweke katika maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.