2015-10-26 15:33:00

Fanyeni mageuzi ya dhati ili kuandika upya ukurasa wa maisha yenu!


Miaka hamsini iliyopita, Mwenyeheri Paulo VI aliwahakikishia Wazingari ambao wamekuwa wakiangaliwa kwa jicho la kengeza na jamii nyingi kwamba, Kanisa linawapenda, linawaheshimu na kuwathamini na kwamba, litaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwao katika shughuli na mikakati yake ya kichungaji. Tangu wakati huo, Jumuiya ya Wazingari ikajenga imani na matumaini kwa Kanisa, kiasi cha kuanza mchakato wa Uinjilishaji, huduma za kijamii na kitamaduni kwa ajili ya watu hawa ambao wametawanyika sehemu mbali mbali za dunia.

Ni ushuhuda uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu 26 Oktoba 2015 alipokutana na mahujaji zaidi ya  5, 000 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliofika mjini Roma kama kielelezo cha kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 tangu Jumuiya ya Wazingari ilipokutana na kuzungumza kwa mara ya kwanza na Khalifa wa Mtakatifu Petro mjini Pomezia, Italia. Kutokana na mwelekeo huu chanya kutoka kwa Kanisa kumekuwepo na ongezeko kubwa la miito mitakatifu kutoka ndani ya Jumuiya, kielelezo cha imani, matumaini na upatanisho.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Jamii inayowazunguka inahitaji kuona mashuhuda wazi wa tunu msingi za Kiinjili, ili kukuza na kudumisha miito mitakatifu; kwa kuwasindikiza watu waliowekwa wakfu katika hija ya maisha, ambayo wakati mwingine inasheheni furaha, magumu na majonzi. Shida na magumu wanayokabiliana nayo katika maisha, kwa kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na Kanisa pamoja na Serikali husika, ili kuiwezesha Jumuiya hii kupata fursa za ajira pamoja na huduma msingi ili kudumisha utu na heshima ya binadamu sanjari na kuzingatia sheria za nchi na haki msingi za binadamu. Kila mtu anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kiraia.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa Jumuiya hii kufanya mageuzi makubwa katika maisha yake, ili kuanza kuandika ukurasa mpya unaojiondoa katika misingi ya maamuzi mbele, woga usiokuwa na mashiko na ubaridi; mambo ambayo kimsingi ni chanzo cha ubaguzi na nyanyaso za kila aina. Hakuna mtu anayepaswa kubaguliwa wala kutengwa, bali kukumbatiwa na huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo.

Ni wakati muafaka wa kuondokana na ubinafsi, ili kujenga na kudumisha utu, umoj, udugu na mshikamano wa kweli, kwa kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni Wakristo wema na mashuhuda wa tunu msingi za Kikristo. Mbele yao wana Mtakatifu Zeffirino Gimènez Malla, shuhuda wa unyenyekevu na ukweli; mwamini aliyeonesha ibada kwa Bikira Maria, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake na leo hii anatambulika kuwa ni “Shuhuda wa Rozari. Mtakatifu huyu ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya kiroho na kitamaduni na kikabila kwa kuzingatia tunu msingi zinazowaunganisha kama Jamii moja.

Baba Mtakatifu anawataka kuhakikisha kwamba, kweli wanatekeleza sheria na kanuni mahalia; kwa kukuza na kudumisha karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu; tayari kuendeleza utu na heshima yao kama binadamu; mambo yanayojikita katika elimu makini itakayowawezesha kupata fursa za ajira. Wazazi wasiwe ni kikwazo cha watoto wao kwenda shule; na wazazi pia watekeleze dhamana yao kikamilifu kwa njia ya mifano bora ya maisha, tayari kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa mstaafu Benedikto XVI, daima wamonesha upendeleo wa pekee unaotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya kuisaidia Jumuiya ya Wazingari, kwa kutambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.