2015-10-26 08:40:00

Bikira Maria ni Sanduku la Agano kati ya Mungu na binadamu!


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi pendevu cha hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo! Karibu, tuendelee kuutegea sikio waraka wa Baba Mtakatifu Francisko maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka mtakatifu wa Jubilei kuu ya  huruma ya Mungu, tutakaouadhimisha kuanzia hapo tarehe 8 Desemba 2015 na kuuhitimishwa katika Sherehe ya Kristo Mfalme mwaka 2016.

Pamoja na mambo mengine ambayo Baba Mtakatifu ndani ya Misericordiae vultus alitufundisha katika kipindi kilichopita, ni pamoja na nafasi ya Mama Bikira Maria katika mpango mzima wa huruma ya Mungu kwa  wanadamu. Mama  Bikira Maria kwa huruma kuu ya Mungu amejaliwa kulibeba fumbo kuu la huruma ya Mungu, ndiye Kristo Yesu. Na katika ule utenzi wake, Baba Mtakatifu alisema, Mama Bikira Maria aliisifu huruma hiyo ya Mungu kuwa ni ya nyakati zote; aliposema, huruma yake hudumu kizazi hata kizazi. Baba Mtakatifu anatualika tutafakari fumbo hili kuu kwani mimi na wewe pia tumejumuishwa katika vizazi ambavyo vinatajwa na Mama Bikira Maria katika utenzi ule maarufu aliouimba alipokuwa nyumbani kwa Elizabeti.

Mpendwa msikilizaji, kwa namna ya pekee tena leo, Baba Mtakatifu anaendelea kututafakarisha juu ya huyohuyo Mama yetu Bikira Maria katika safari ya ukombozi. Jambo moja kubwa sana analotufundisha Mama Bikira Maria ni kwamba, huruma ya Mungu haina mipaka. Pale Msalabani, Mama Maria pamoja na Yohane (mwanafunzi aliyependwa), waliyashuhudia maneno ya msamaha yaliyotamkwa na Yesu. Baba Mtakatifu anasema, ‘maneno yale ulikuwa ni udhihirisho wa kipeo cha juu kabisa ambacho huruma ya Mungu huweza kufikia. Mama Maria anashuhudia kwamba, huruma ya Mungu haina mipaka na inaelekezwa kwa watu wote bila ubaguzi.

Baba Mtakatifu anaendelea kumwelezea Mama Bikira Maria kwa mwangwi wa sala ile ya ‘Salamu Malkia’, sala ambayo ni ya zamani sana lakini daima ni mpya. Kwa sala hiyo tunaendelea kumwomba  asichoke kutuelekezea macho yake ya huruma, ili tustahili kuutafakari uso wa huruma wa Yesu Mwanawe.

Sala yetu pia inaelekezwa kwa watakatifu na wenyeheri wote, ambao walipokuwa bado hapa duniani, waliifanya huruma ya Mungu kuwa ndiyo utume wao ; na kwa mfano wa maneno yao, matendo yao na maisha yao mazima, waliitangaza huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anapowatazama watakatifu kama wajumbe wa huruma ya Mungu, kwa namna ya pekee anamkumbuka Mtakatifu Faustina Kowalska ambaye ni Mtume wa huruma ya Mungu kwa namna ya pekee kabisa.  Kristo Bwana alimteua Sista Faustina kuingia katika undani wa huruma ya Mungu. Yeye atuombee neema tunazohitaji ili nasi tuweze kuenenda katika mwanga wa huruma ya Mungu na tudumu thabiti katika upendo na matumaini kwa huruma hiyo kuu ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko ndani ya Misericordiae vultus anaendelea kufafanua mwelekeo wa Jubilei hiyo Kuu ya huruma ya Mungu akisema « kwa hiyo ninaiweka Jubilei hii ya pekee, ili tuweze kuiishi huruma ya Mungu katika maisha yetu ya  kila siku. Tuiishi  huruma ambayo Baba Mungu hutukirimia sisi sote ». Anaendelea kusema Baba Mtakatifu “ katika mwaka huo Mtakatifu wa huruma ya Mungu, tumruhusu Mungu atushangaze ! Mungu wetu hachoki kutufungulia milango ya moyo wake, huku akizidi kusema kuwa anatupenda na anataka tulishiriki pendo lake.

Kanisa linaona uhitaji wa muhimu kabisa kutangaza huruma ya Mungu. Maisha ya Kanisa yanapata maana tu pale ambapo Kanisa linakuwa kweli mtangazaji wa ujumbe wa Huruma ya Mungu. Kanisa linajua kwamba wajibu wake wa msingi ni kumuingiza kila mtu katika Fumbo kuu la huruma ya Mungu kwa kuutafakari uso wa Kristo, kwa nyakati zote, hasa zile nyakati za matumaini na zile nyakati zenye ishara tele za mikanganyiko.

Kanisa linaalikwa kwa namna ya pekee zaidi kuwa shuhuda wa kweli wa huruma  ya Mungu, kwa njia ya kuiamini na kuuiishi huruma hiyo ya Mungu kama kiini cha ufunuo wa Kristo Yesu. Kutoka katika moyo wa Utatu Mtakatifu, na kutoka katika undani wa fumbo la Mungu, mto wa huruma ya Mungu hutiririka bila kukoma. Ni chemchemi  ambayo haitakauka kamwe hata kuwe  na watu kiasi gani wanaoikimbilia. Kila wakati lazima kuna fulani mwenye kuhitaji na lazima aikimbilie chemchemi hiyo kwa sababu huruma ya Mungu haina kikomo.

Anakaza  kusema Baba Mtakatifu Francisko, katika mwaka huo wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, Kanisa lihubiri Neno la Mungu linalotoa ujumbe mwangavu wa msamaha, nguvu, msaada na upendo. Kanisa lisichoke kamwe kuonesha huruma, na liwe na saburi katika kuonesha huruma na faraja. Anasisitiza Baba Mtakatifu, Kanisa liwe sauti ya kila mmoja na lirudie kwa ujasiri usiokoma maneno ya Mzaburi asemapo « Ee Bwana kumbuka rehema zako na fadhili  zako, kwa maana zimekuwepo tokea zamani » (Zab. 25 :6).

Hadi kufikia hapo mpendwa msikilizaji tumefikia tamati ya Ujumbe huu wa Mwaka Makatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu kama ulivyotangazwa na Baba Mtakatifu Fransisko. Baba Mtakatifu sambamba na ujumbe huu anatualika kusali kwa dhati ya moyo Rozali ya Huruma ya Mungu. Tunawatakieni nyote makaribisho mema na maadhimisho mema ya Mwaka wa Huruma ya Mungu na Mungu wetu aliye mwingi wa huruma aiongoze miguu yetu katika njia ya amani.

Kutoka katika Studio za Radio vatican, ni mimi Pd. Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.