2015-10-25 14:24:00

Mababa wa Sinodi ya familia wamehitimisha maadhimisho na kufungua ukurasa mpya!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 25 Oktoba 2015 amehitimisha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, yaliyokuwa yanaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo” kwa Ibada ya Misa takatifu, iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia huruma na ubaba wa Mungu anayewajali watu wake na kikomo chake kinajionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu katika Agano la kale amejifunua kuwa ni Baba wa wote, anayekomboa, anayehurumia na kuwasindikiza waja wake katika shida na mahangaiko yao, ikiwa kama watu wake wataendelea kuwa waaminifu, huku wakimtafuta kwa moyo wa toba; atawakirimia uhuru na kuwaonjesha umoja na mshikamano unaojikita katika furaha. Wokovu wa Mungu ni kielelezo cha madimbwi ya furaha kutoka kwa watu wake wanaoweza kupokea neema hii inayovuka mipaka ya kibinadamu.

Yesu ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu ambaye ameyatekeleza yote haya kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, kwa kujitwalia hali ya binadamu katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Kutokana na mwelekeo huu, Yesu amekuwa kweli ni kiungo muhimu cha upatanisho katika Agano jipya na chanzo cha ukombozi.

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia kwamba, Bartimayo kipofu alionjeshwa huruma na upendo wa Yesu, ingawa Yesu mwenyewe alikuwa kwenye safari muhimu sana katika maisha na utume wake, lakini aliweza kusimama na kusikiliza kilio cha Bartimayo kipofu, akaguswa na mahangaiko yake kiasi cha kukutana naye uso kwa uso na kumuuliza swali la msingi na anapata jibu muafaka kwamba, “Bwana nataka kuona”. Imani ya Bartimayo kipofu, inampatia neema ya kuweza kuona tena mwanga unaobubujika kutoka kwa Yesu Kristo, kielelezo cha imani tendaji.

Yesu bado anapenda kuzungumza na kila mwamini kutoka katika undani wa maisha yake lakini anawataka kuwa na ujasiri unaojikita katika imani, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Yesu anayewainua kutoka katika magonjwa na mahangaiko yao ya ndani. Hii ndiyo changamoto endelevu kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, linawaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kuokoa.

Ni mwaliko kwa familia ya Mungu kuonesha huruma ya Mungu kwa watu wanaoishi katika umaskini na kinzani za dunia hii. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni wakati wa huruma ya Mungu! Wafuasi wa Kristo waguswe na mahangaiko pamoja na mateso ya walimwengu, tayari kusimama na kuwasikiliza kwa moyo wa ukarimu kama alivyofanya Yesu mwenyewe! Wajifunze kutoka kwa Yesu mwenyewe kuwa na moyo wa huruma na mapendo, wanapotembea katika jangwa la maisha ya wanadamu, ili kuweza kusimika imani katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kuwaondoa kutoka katika majangwa ya maisha, tayari kuwaonjesha ile furaha na neema inayobubujika kutoka kwa Yesu mkombozi wa dunia.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuondokana na kishawishi cha kuwa na mwongozo tofauti wa maisha, kwa kutokuwa na uvumilivu pamoja na kuendelea kuwa kikwazo kwa watu wanaotaka kumwona na kuzungumza na Yesu kama inavyojidhihirisha katika Maandiko Matakatifu. Yesu anataka kuwashirikisha wote katika huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka; hasa zaidi wale wanaopiga kelele kuomba huruma yake, kwani wanatambua kwamba, wana kiu ya wokovu unaotolewa na Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Bartimayo kipofu alibahatika kuona na hatimaye, akajiunga na Yesu, kama walivyofanya Mababa wa Sinodi wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya familia. Kanisa limetembea pamoja kwa kusali, kutafakari na kushirikishana mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Injili ya Kristo, ili kutangaza uzuri, utakatifu na upendo wa familia.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Kristo ili awawezeshe kuwa na mwelekeo mpya wa kuponya na kuokoa, ili kueneza mwanga wake bila kuvurugwa na dhambi, bali kutafuta, ili hatimaye, kuona utukufu wa Mungu unaojidhihirisha kwa mtu aliye hai!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.