2015-10-25 08:03:00

Askofu Ngalalekumtwa: Kanisa linasimamia: Uzuri na utakatifu wa familia


Maana ya Familia ya familia, uzuri, utakatifu, malengo na wajibu wake ni kati ya mambo ambayo Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia wameyajadili kwa kina na mapana anasema Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican. Mababa wa Sinodi wamekazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa malezi ya awali na endelevu sanjari na majiundo makini kwa wanandoa ili waweze kutekeleza dhamana, wajibu na wito wao ndani ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Askofu Ngalalekumtwa ambaye anashiriki maadhimisho ya Sinodi ya familia kwa miaka miwili mfululizo anakaza kusema, Yesu Kristo anaita, anawafunda na kuwatuma wanandoa ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, kumbe, ndoa ni wito na jambo ambalo linapaswa kupewa uzito wa pekee na waamini katika hija ya maisha yao ya kila siku. Ndoa kati ya Wakristo, yaani bwana na bibi imepewa hadhi ya kuwa Sakramenti, kielelezo makini cha upendo mkamilifu kati ya bwana na bibi, wakati wa raha na shida, wakati wa magonjwa na mahangaiko ya maisha.  Sakramenti ya Ndoa inawawezesha wanandoa kupokeana na kusaidiana kama Malaika walinzi katika hija ya maisha, ili kwa pamoja, wakisaidiana pia na watoto wao waweze kufikia utakatifu wa maisha.

Kanisa linakazia uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia. Hii inatokana na ukweli kwamba, Ndoa ni Sakramenti ya Kanisa; ni chombo cha utakaso na njia ya wokovu. Mababa wa Kanisa wanakaza kusema, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya utakatifu, haki na amani. Hapa ni mahali ambapo wanandoa wanapaswa kujisadaka, tayari kulisifu, kulitukuza na kulishuhudia Fumbo la Utatu Mtakatifu linaloambata umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.