2015-10-23 10:15:00

Waamini wana matumaini makubwa kutoka kwenye Sinodi ya Familia!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Jimbo kuu la Mwanza limeadhimisha Mwaka wa Familia, uliohitimishwa rasmi hapo tarehe 22 Machi 2015. Maadhimisho haya ni mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo kuu la Mwanza iliyohitimishwa kunako mwaka 2002. Kumbe, Mwaka wa Familia ni matunda pia ya maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kilele cha Jubilei ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na mwendelezo wa maazimio ya Sinodi za Maaskofu wa Afrika.

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, ni matumaini yake kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo” imekuwa ni fursa kwa Mababa wa Sinodi kuangalia kwa kina na mapana kuhusu wito na utume wa familia; kwa kupambanua kwa weledi na roho ya Kikatoliki changamoto zinazolikabili Kanisa na wanakanisa katika ujumla wao katika ulimwengu mamboleo.

Askofu mkuu Ruwaichi anafafanua zaidi kwamba, ulimwengu mamboleo unaendelea kushuhudia kucharuka kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini kwa bahati mbaya, waamini wengi bado hawajalelewa kiasi cha kuweza kukabiliana na maendeleo haya kwa uwajibikaji mpana zaidi sanjari na kutumia fursa za uvumbuzi na maendeleo haya kikamilifu kwa ajili ya ustawi wa wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.