2015-10-23 12:17:00

Kanisa linataka kuendelea kuwa ni sauti ya wanyonge katika utunzaji wa mazingira


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika tafakari yake kuelekea maadhimisho ya mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi maarufu kama Cop21 utakaofanyika  mwezi Desemba 2015 huko Paris, Ufaransa anasema kwamba, Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, "Laudato si" ni mchango mkubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kutafuta mafao na ustawi wa wengi. Mada ya mazingira ni jambo linawagusa watu wote kwani hapa: haki na amani; utu na heshima ya binadamu pamoja na zawadi ya maisha, vinaweza kuwekwa rehani.

Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko unajikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa na wala si kwa ajili ya kampeni ya watu wanaotetea mazingira peke yao. Ni mchango unaopata chimbuko lake kutoka katika Nyaraka mbali mbali za Kanisa kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa tangu  ule Waraka wa Rerum Novarum, Mwanzo mpya, ulioandikwa na kuchapishwa na Baba Mtakatifu Leo wa kumi na tatu, kunako mwaka 1891.

Kardinali Turkson anakaza kusema, Waraka wa Baba Mtakatifu kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, umeisaidia Jumuiya ya Kimataifa kutambua zaidi athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuvalia njuga suala zima la utunzaji wa mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi, lakini zaidi maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ndio waathirika wakuu. Binadamu anapaswa kutafuta njia bora zaidi za utunzaji wa mazingira kwani shughuli mbali mbali za binadamu zinaendelea kuchangia katika uharibifu wa mazingira, nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko anataka utunzaji bora wa mazingira ile ni kati ya ajenda kubwa zinazojadiliwa na kutekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu. Kwa Waraka huu, Kanisa linataka kuendelea kuwa ni sauti ya wanyonge; watu wanaopoteza maisha yao kila siku kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchim, lakini hakuna anayewasikiliza, kwani watu wanaangalia masilahi yao binafsi. Wadau mbali mbali katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati unaotekelezeka katika utunzaji bora wa mazingira, wakati wa mkutano wake huko Paris, Ufaransa. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kuwajibika barabara, kwa ajili ya mafao ya wengi, hata ikibidi kwenda kinyume na sera zinazojikita katika ubinafsi na masilahi ya watu au mataifa machache.

Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kufanya majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wote. Mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira huko Paris, usipofikia malengo yake ni kielelezo cha kushindwa pia kwa mikutano mingi ya kimataifa inayotarajiwa kimsingi kujikita katika ustawi na maendeleo ya wengi. Kanisa Katoliki katika Mafundisho Jamii linakazia kuhusu umuhimu wa mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanuni auni; mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maisha ya viumbe hai yako hatarini, kumbe ni jukumu la wote kulinda zawadi ya uhai.

Ustawi na maendeleo ya wengi kwa siku za usoni, uko mikononi mwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, ikiwa kama watafanikiwa kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya mafao ya wengi, dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Waraka wa Baba Mtakatifu kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, utaendelea kuwa ni dira na mwongozo kwa ajili ya mafao ya wengi. Maskini wa dunia wanasubiri kuona cheche za mshikamano kutoka kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, kwani wote ni raia wa ekolojia. Baba Mtakatifu anaendelea kusali, dhamana muhimu sana katika maisha ya watu na kwamba, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali, ili mkutano wa kimataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa uweze kufanikiwa na kuleta matunda yanayokusudiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Kwa kumtegemea na kujiaminisha kwa Mungu, Kardinali Peter Turkson anasema hakuna kinachoweza kushindikana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.