2015-10-23 11:25:00

Kanisa lina dhamana ya kuchangia ustawi na maendeleo ya mtu mzima!


Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba linamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kufanikisha hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao, alipokuwa njiani kuelekea Marekani. Ni hija ambayo imeamsha ari na moyo wa kimissionari unaowakumbatia wote, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni bandari salama kwa wote wanaokimbilia ulinzi na tunza yake ya kimama. Baba Mtakatifu Francisko kwa hakika amekuwa ni chombo na mjenzi wa daraja kati ya Marekani na Cuba, kiasi kwamba, leo nchi hizi mbili zimerejesha tena uhusiano wao wa kidiplomasia baada ya kusigana na kulumbana kwa takribani miaka hamsini ambayo imekuwa ni shida na mahangaiko makubwa kwa wananchi wa pande hizi mbili.

Maaskofu wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Cuba kutafakari kwa kina na mapana mchango wa Baba Mtakatifu Francisko katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Cuba katika ujumla wao. Baba Mtakatifu kwa hakika ameonesha ile sura na karama ya Mchungaji mwema. Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Cuba na Marekani yamefungua malango kwa Cuba katika medani mbali mbali za Jumuiya ya Kimataifa, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cuba.

Baraza la Maaskofu linawaalika kwa namna ya pekee waamini na wananchi katika ujumla wao, kutambua na kuthamini mchango wa Kanisa mahalia katika ustawi na maendeleo ya Cuba katika ujumla wake. Kanisa ni jumuiya ya waamini wanaoamini, kukiri na kushuhudia ukuu wa Kristo Yesu, changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anashiriki kikamilifu katika ujenzi na ustawi wa Kanisa la Kristo.

Kanisa litaendelea kumhudimia mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa pamoja na katika medani mbali mbali za maisha: kisiasa, kiuchumi na kijamii, kwani huu si uwanja wa wanasiasa peke yao, wanapaswa kusaidiwa na hekima na busara ya kimungu. Dini ina mchango na nafasi yake katika ustawi na maendeleo ya binadamu na wala si bangi kama ilivyokuwa imezoeleka kusikika wakati wa utawala wa kikomunisti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.