2015-10-21 09:54:00

Sinodi ni kielelezo cha ujasiri, ukweli na uwazi!


Askofu Bruno Forte, Katibu mahusus wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, tangu mwanzo, Baba Mtakatifu Francisko amewahamasisha Mababa wa Sinodi kuwa na ujasiri, ili kuzungumza katika ukweli na uwazi, ili kushuhudia Kanisa linalojadiliana, Kanisa ambalo liko hai na linawajibika katika maamuzi yake.

Ni majadiliano yanyofanyika katika umoja na utofauti, utajiri mkubwa wa Kanisa Katoliki na wala hiki si kielelezo cha kinzani na migawanyiko kama ambavyo baadhi ya watu wanataka kuamini! Mababa wa Sinodi wanaunganishwa na Imani kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume; wanawajibika mbele ya Mwenyezi Mungu na ndugu zao katika Kristo; mambo yanayowaunganisha kwa dhati Mababa wa Sinodi huku wakiendelea kuambata Neno la Mungu, Mafundisho tanzu ya Kanisa, Sakramenti na Nidhamu.

Mababa wa Sinodi wanaendelea kufanya upembuzi yakinifu kuhusu uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia unaojikita katika: Umoja na upendo; Ukarimu na mshikamano; Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa; Maadili na utu wema. Utume wa maisha ya ndoa na familia hauna budi kuwa ni chombo kinachowasindikiza wanandoa katika safari ya imani, matumaini na mapendo; kwa kuwasikiliza na kushirikishana karama, dhamana na majukumu, tayari kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kristo.

Kila mwamini anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa pamoja na kupewa nafasi ya kushirikisha karama na mapaji yake kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Ushiriki wa waamini unatofautiana, kumbe wale wanaoogelea katika mitikisiko ya imani wanapaswa kusindikizwa na kusaidiwa na Mama Kanisa ili kuendelea kushikamana na wengine licha ya mapungufu na madhaifu yao.

Maadhimisho ya Sinodi ya familia ni chanda na pete na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kwamba, mikakati ya kichungaji itakayotolewa na Mama Kanisa kuanzia sasa inapaswa kumwilishwa na kuambata huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kuokoa: Kanisa linapania kwa namna ya pekee, kutangaza na kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu kwa watu wa mataifa katika haki na ukweli. Kanisa linatambua kwamba, huruma ya Mungu ni kiini na moyo wa maisha ya Kikristo.

Mababa wa Sinodi wanatafakari jinsi ya kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini pamoja na kuendelea kuambata Mafundisho tanzu ya Kanisa katika maisha na utume wa familia. Maadhimisho haya yamekuwa ni fursa ya kusikiliza wanafamilia wakishuhudia uzuri, utakatifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia. Ikumbukwe kwamba, hata wakleri wanatambua mengi yanayoendelea katika maisha ya ndoa na familia kwani ni kundi ambalo liko bega kwa bega na familia katika maisha na utume wake anakaza kusema Askofu Bruno Forte. Mababa wa Sinodi wana dhamana na wajibu kwa familia, kumbe, mchango wao ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wanataka kuendelea kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kujikita katika Mafundisho tanzu ya Kanisa, Injili ya Kristo, huruma ya Mungu; haki na ukweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.