2015-10-21 12:00:00

Ndoto ya Mt. Gaspar inaendelea kuzaa matunda!


Kanisa tarehe 21 Oktoba 2015 linaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, muasisi wa Shirika la Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu, ambalo kwa mwaka 2015 linasherehekea Jubilei ya miaka 200 tangu lilipoanzishwa na kwamba, ndoto yake ya kusambaza huruma na upendo wa Mungu kwa kusikiliza kilio cha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni ma jamii inaendelea sehemu mbali mbali za dunia. Katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 ya C.PP.S., Kanda ya Tanzania, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma katika mahubiri yake alipembua kwa ufupi historia ya maisha na utume wa Mtakatifu Gaspar.

Kwa hakika, Gaspar alikuwa ni Padre mwaminifu kwa Kanisa, akayakabilia mateso, dhuluma na nyanyaso kwa moyo mkuu na kwa njia ya msaada na tunza ya Bikira Maria. Alikuwa ni mhubiri hodari wa Neno la Mungu na mtume mahiri wa Damu Azizi ya Yesu, aliyejitahidi kusikiliza kilio cha damu ya maskini, akawa ndugu, rafiki na mlinzi wao!

Gaspar akiwa bado Padre kijana kabisa alijikuta anapelekwa uhamishoni kwa kukataa kula kiapo cha utii kwa Mfalme Napoleone Buonaparte. Gaspar akasimama kidete na kukubali kupelekwa uhamishoni, ambako alifanya tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Msalaba na mateso ya Kristo, chemchemi ya: amani, upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu. Alipotoka uhamishoni, akaanzisha Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, hapo tarehe 15 Agosti 1815 na kuliweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria.

Gaspar akatoa kipaumbele cha pekee kwa Bikira Maria katika maisha na utume wa Shirika lake, changamoto anasema Askofu mkuu Kinyaiya kwa watoto na waamini kwa ujumla kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria; kielelezo cha uaminifu, upendo na huduma makini kwa jirani. Ni kielelezo cha Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, mwaliko kwa C.PP.S, Tanzania kufungua Parokia kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma, ili kuendeleza utume kwa vijana.

Wamissionari wa C.PP.S pamoja na mafanikio makubwa waliyokwisha kupata kutokana na huduma katika sekta ya afya, elimu, maji na maendeleo jamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira, wanahimizwa kusonga mbele kwa kujikita katika maboresho ya huduma hizi na pale inapowezekana kuanzisha huduma nyingine kadiri Roho wa Bwana atakavyowawezesha.

Askofu mkuu Kinyaiya anakaza kusema, Jubilei ni kielelezo cha furaha, toba na msamaha. Ni wakati wa kujipanga na kujiwekea malengo kwa siku za usoni. Shida na changamoto ni sehemu ya maisha ya binadamu na kamwe zisiwakatishe tamaa, bali wawe na nguvu ya ziada kama Kanda ya C.PP.S nchini Tanzania. Siri kubwa ya mafanikio katika maisha na utume wao ni kumtumainia Yesu Kristo; kujikita katika maisha ya kijumuiya na kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatangazia watu huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo. Wamissionari wawe ni watu wa huduma inayofumbata sala na tafakari ya Neno la Mungu.

Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa C.PP.S ni kielelezo kwamba, ndoto ya Gaspar inaendelea kumwilishwa sehemu mbali mbali za dunia katika maisha na utume wa Shirika. Ili kufikia kilele hiki, Wanashirika walipata nafasi ya kutafakari utume na maisha yao kwa kipindi cha miaka mitatu huku wakiongozwa na mada: Maisha, historia na karama ya Shirika; Upatanisho; Majibu ya kilio cha damu kutokana na watu wanaoelemewa na magonjwa, ujinga, umaskini na mpasuko wa imani.

Kunako mwaka 2014 mkutano mkuu wa wakuu wa Shirika la C.PP.S wakaamua kwamba Tanzania inapoadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na ushuhuda wa Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, iwe ni Kanda inayojitegemea, ili kuendeleza ndoto ya Mtakatifu Gaspar kwa kujikita katika: Utume, maisha ya kijumuiya na tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu. Leo hii Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu wanatekeleza utume wao Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Jimbo Katoliki Morogoro, Jimbo Katoliki Ifakara, Jimbo kuu la Dodoma na Jimbo la Singida, mahali walipoanzia huduma yao ya kimissionari kunako mwaka 1968, huko Manyoni. Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wanaandika historia ya Shirika lao kwa machozi ya furaha.

Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya hapo tarehe 8 Agosti 2015, Padre Egidius Seneda alisoma tamko la Mheshimiwa Padre William Nordenbrock mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu duniani. Katika hotuba yake ya shukrani amelipongeza Kanisa la Tanzania kwa kuwakubali na kuwapokea Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kutoka Italia waliokuja kutekeleza dhamana na azma ya Uinjilishaji wa kina: kwa kugusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; waamini walei kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Wamissionari katika kukuza huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa wamissionari wenyewe waliojisadaka katika huduma za kichungaji sanjari na kukuza miito kwa wazalendo, leo hii Shirika nchini Tanzania lina Wamissionari zaidi ya 70.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.