2015-10-21 13:43:00

Katekesi ya Papa : upendo na uaminifu ni msingi wa familia


Baba Mtakatifu Francisko , mapema Jumatano hii,  kama kawaida alitoa Katekesi kwa mahujaji na wageni, wakiwa katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican. Aliangalisha tena katika Mada ya Familia , leo akizama katika haja ya wanandoa kuzingatia na kuishi ahadi yao ya  upendo na uaminifu kama msingi wa familia. Maelezo ya Papa ilikuwa ni mwendelezo wa mada ya wiki iliyopita ambamo alizungumzia juu ya  ahadi za wazazi kwa watoto wao wanaojaliwa na Maulana.  Jumatano hii, ametoa  mwaliko kwa wanandoa wote, kwa pamoja, kutafakari kwa kina  ahadi ya upendo na uaminifu kati yao, kama  msingi wa maisha yote ya familia.

Papa Francisco ameasa, ingawa ahadi hizi kwa siku hizi, zinachukuliwa kama namna  fulani ya  kuwa kinyume na uhuru wa mtu binafsi, ukweli unaendelea kubaki  kwamba,  uhuru ni sehemu ya umbo  endelevu katika  uaminifu wetu kwa uchaguzi na ahadi tunazozifanya sisi wenyewe katika maisha. Papa amesisitiza kwamba, uaminifu huwa thabiti, kwa  juhudi zetu wenyewe katika shughuli na vitendo vya kila siku, katika   kutimiza ahadi zetu. Na ametaja uaminifu katika ahadi zetu, huonyesha hadhi na heshima ya mtu. Na Hakuna shule zaidi ya  kutufundisha uaminifu kuliko ndoa na familia, ambao ni katika mpango wa Mungu, na  baraka zake  kwa dunia yetu.

Maelezo ya Papa pia yalirejea katika waraka wa  Mtakatifu Paulo, ambamo anaeleza  kwamba upendo unaounganisha familia, hulenga katika kifungo cha upendo kati ya Kristo na Kanisa, kutekeleza na kuimarisha ahadi ya familia. Papa alimalizia na Ombi kwa Bwana ili kwamba katika siku hizi ambamo kuna Sinodi kwa ajili ya familia, kwa ubunifu na katika kujali upungufu wa uaminifu, Kanisa liweze kutekeleza na kuimarisha ahadi ya familia ambamo Bwana hutimiza ahadi zote.

Baada ya Katekesi Papa alisalimia makundi  mbalimbali ya watu waliofika kumsikiliza, yakiwemo makundi makubwa kutoka Uingereza, Sweden,  Ireland, Norway,  China, Indonesia, Japan,  Malaysia, Canada na Marekani. Na kwa namna ya kipekee alitoa salaam zake kwa washiriki wa Mkutano wa Kituo Kikuu cha Mashemasi , na pia alitoa shukurani zake kwa kwaya ya Nagasaki iliyotumbuiza na kutoa shuhuda zake katika imani. Kwao wote aliwapa Baraza zake za Kipapa.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.