2015-10-21 08:59:00

Kanisa ni sauti ya kinabii kwa wanyonge na wote wanaoteseka!


Vita, kinzani za kisiasa, kijamii na kidini; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na myumbo wa uchumi kimataifa ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuchangia makundi makubwa ya watu kuzikimbia nchi zao, ili kutafuta usalama na uhakika wa maisha, licha ya kutambua kwamba, wanakabiliana na kifo uso kwa uso. Wahamiaji na wakimbizi ni changamoto kubwa na endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa inayohitaji sera na mikakati inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kushughulikia changamoto ya wakimbizi kwa kujikita katika mshikamano wa kimataifa unaoongozwa na kanuni auni, ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Viongozi wa kimataifa watafute kwanza kabisa mafao ya wengi badala ya kufumbia macho changamoto ya wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kupoteza maisha yao baharini, jangwani na kwenye mipaka ya nchi ambayo kwa sasa inafungwa kwa kuhofia makundi ya wahamiaji, kwa kisingizio cha usalama wa nchi.

Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, hivi karibuni ametembelea kambi za wakimbizi na wahamiaji nchini Ugiriki, ili kujionea mwenyewe hali halisi, tayari Kanisa kuendelea kutoa msaada wa hali na mali, ili kuwajengea wakimbizi na wahamiaji matumaini, licha ya magumu wanayokumbana nayo kwa sasa. Anasema, hali ya wakimbizi ni mbaya sana, kwani wengi wao hawana mahitaji muhimu na wanalazimika kutembea mwendo mrefu huku wakiwa wamebebana na watoto wao wadogo.

Kardinali Tagle anakaza kusema, matatizo, changamoto na matumaini ya wakimbizi na wahamiaji ni kati ya mada ambazo zimechambuliwa na Mababa wa Sinodi ya familia, ili kuliwezesha Kanisa kuwa kweli ni sauti ya kinabii kwa watu wasiokuwa na sauti, hawa ndio wahamiaji na wamkimbizi wanaonyanyasika na kudhulumiwa na kwamba, utu na heshima yao vinawekwa reheani kana kwamba si binadamu. Mababa wa Sinodi kutoka Afrika, Asia na Ulaya wameshirikisha magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Wakimbizi ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi kwa hekima na busara na Jumuiya ya kimataifa, kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika sera na mikakati kwa wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.