2015-10-21 15:32:00

Bartimayo kipofu na vituko vyake! Utachoka na roho yako!


Ndugu yangu! “Ombaomba au Yalamaskini” “Akina yakhe pangu pakavu tafadhali tia mchuzi” ni watu walemavu, viwete, vipofu wanaoomba kusaidiwa au wakati mwingine wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao. Kwa kawaida Ombaomba wanasimama kando ya barabara au penye makutano ya watu wakisubiri wasamaria huruma. Ombaomba ina tija kidogo sana na isiyo ya hakika. Siku nyingine Ombaomba anabahatika kupata ridhiki kidogo, lakini wakati mwingine hapati chochote anabaki akipiga miayo! 

Kila Ombaomba analo lake moyoni, kwani siyo wote wanaosimama kando ya barabara kuomba ni vilema. Wengine wanaweza kuwa vibaka. Leo tutamshuhudia Ombaomba mmoja kipofu aliyeketi kijiweni pake pembeni mwa barabara jinsi alivyopewa shavu la kiutu-uzima hadi akaacha kabisa kukaa kijiweni kuomba yalamaskini. Ili kuweza kuelewa siri ya mafanikio yake, hebu tuone kwanza mazingira yaliyopelekea kituko hicho.

Yesu yuko safarini akitokea Galilea kwenda Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi. Akiwa safarini alikuwa pia anatoa sera mbalimbali juu ya maadili ya maisha kwa wale waliokuwa wanamfuata. Katika dominika tatu mfululizo tumeona sera za maadili alizotoa. Mosi juu ya maadili ya ndoa yaani kutalikiana mke kunavyoathiri familia hadi leo. Pili, juu ya mali na utajiri unavyoweza kumzuia mtu kumtumikia Mungu kama yule kijana tajiri. Tatu ni masuala ya ukuu unavyoweza kusababisha mpasuko katika jumuia.

Leo Msafara wa Yesu umetua Yeriko lakini unapitiliza kwenda Yerusalemu umbali wa kilometa ishiri na saba toka hapo Yeriko. Kama ilivyoandikwa: “Wakafika Yeriko, hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko.” Imesemwa pia kwamba katika msafara huu Yesu “alikuwa pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa.” Makundi haya mawili yanatupatia fundisho fulani la maisha. “Mkutano mkubwa” unamfuata Yesu kwa hoja mbalimbali za binafsi ikiwa ni pamoja na kutaka kuponywa, au hata kula mikate maana “Fuata nyuki ule asali.” Kwa vyovyote watu hawa hawajafunguka macho kutambua kitakachomjiri Yesu huko Yerusalemu. “Wanafunzi wake” walionekana kufunguka macho kidogo, kwani wameshaambiwa kuwa huko Yerusalemu kutakuwa na kimbembe. Yesu atashikwa, anateswa na kufa. Hivi wanajua kwamba hawaelekei kwenye ushindi na ukuu wa Bwana wao bali kwenye kushindwa.

Yesu na msafara wake wanapotoka tu nje ya mji na kuanza safari wanakutana na kijiwe cha Ombaomba mmoja kipofu aitwaye “Mwana wa Timayo, Bartimayo.” Jina hili ni la ukoo linachanganya kidogo kwani linajirudia, yaani “Mwana wa Timayo, na Bar-Timayo” ambapo “Bar” maana yake ni Mwana au bin wa Timayo. Kwa hiyo kuna “Mwana wa Timayo,” halafu tena “Bartimayo”  yaani  Mwana wa Timayo. Kulikoni! “Timayo” kwa lugha ya kiebrania lina maana mbili: Mosi, ni heshima, hadhi, ukuu, kufanikiwa na kuthaminiwa katika maisha ya ulimwengu huu. Kwa hiyo Mwana wa Timayo au Bartimayo ni mtu anayefanana na baba yake katika heshima, yaani mwana au mtoto wa yule anayetafuta heshima, hasahasa heshima katika vitu vya ulimwengu huu. Maana nyingine ya Timayo ni uchafu, yaani Mwana wa uchafu. Maana hii ndiyo inayoweza labda kuelezeka hapa linaposisitizwa jina hilo. “Mwana wa Timayo, Bartimayo,” yaani kile kionekanacho machoni pa jamii nzima kuwa ni cha maana, cha ukuu, cha hadhi, na cha heshima, kumbe, kwa kweli ni uchafu na takataka, kwani vitu hivyo vya hadhi ndivyo vinavyotupofusha macho tusiweze kuona njia ya kweli. Yawezekana hata sisi ni wana wa ukoo wa Timayo.

Basi huyo Mwana wa Timayo “alikuwa ameketi kando ya njia.” Upate picha ametandika mgololi wake miguuni, ametulia, kaangalia chini akisubiri Msamaria na Mhaji anayekwenda kuhiji amtupie chochote kitu. Yuko kijiweni “kando ya barabara,” hana malengo zaidi, ameridhika na maisha yanavyoenda, haangalii mbele au juu bali chini kwenye maisha ya sasa na hapa duniani. Yaani amezaliwa, amekua na sasa anasubiri kufa basi. Lakini huyu Mwana wa Timayo, Bartimayo ni kipofu lakini jeuri, kwani anayo masikio makali sana. Sikio lake linaweza kusikiliza na kugundua sauti inayoweza hata kuukonga moyo na roho yake. Kwa hiyo aliposikia minong’ono juu ya mtu fulani wa pekee anapita akielekea Yerusalemu, hapo hakulaza damu. Akapiga kelele na kumwita Yesu kwa jina linalojulikana na wayahudi wote: “Yesu mwana wa Daudi, unirehemu.”

Kwa mwito huo yaonekana kipofu huyu hakuwa na hakika Yesu alikuwa nani. Alifanya kubahatisha  pengine ni mtu fulani wa pekee, pengine ni mfalme, au ni tajiri, ni mtukufu, ni maarufu, na hivi haikosi atakuwa mwana wa Daudi tu anayeweza kumshika shavu la kueleweka. Kadhalika msafara wa Yesu ulikuwa pia na upofu huo fulani, kwani ulimkemea ili anyamaze. Waliweza  kuwa mashabiki waliojidai wana mapenzi mema naye wakajidai kumtuliza asipige kelele. Wanamzuia ili aendelee kuketi kijiweni kando ya barabara aendelee kuomba “Kalaga baho - taabika hapo hapo ulipo.”  Lakini kipofu huyu ni king’ang’anizi kweli kweli, akaendelea kupiga kelele hadi kikaeleweka.

Kilio chake kikamwingia Yesu, akaona afadhali kuanua ngoma juani. Akasimama na kuagiza: “Mwiteni.” Hapa angalieni tena kwa makini, siyo sauti ya Yesu moja kwa moja inayomwita yule kipofu, bali wanatumwa wengine kumwita. Hawa siyo tena wale mashabiki, bali ni wafuasi halisi wa Yesu, wanaotangaza mwito wa Yesu, wanaojali na kusikiliza vilio vya wanyonge, vilio vya wahitaji waliokata tamaa ya maisha. Wafuasi hao ndiyo wanaomwonesha kipofu njia inayoongoza kwa Kristu. Watu aina hiyo hawana lugha mbaya, hawamwoni kipofu kwa jicho bovu la kukatisha tamaa, bali wanamwita kwa maneno matatu tu ya kutia moyo: “Jipe moyo; inuka, anakuita.” kwa Kigiriki ni “Tharsei” maana yake jikaze, uwe na furaha, changamkia masuala. Halafu egeirai ni inuka, amka achana na maisha ya zamani. Phonei, maana yake anakuita.

Sasa tungetegemea kipofu huyu angejitengeneze kidogo na kujitanda vizuri mgololi wake halafu asubiri wamshike mkono kumwongoza kwa Yesu. Hapana! Bwana, anakurupuka mara moja “akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu.” Mgololi wa Bartimayo ulikuwa ndo maisha yake, kwani aliutandaza miguuni pake ili kuombea yala maskini! Na wale wenye vijisenti vyao wakampatia kitu kidogo!. Anaposikia anaitwa hapo sasa “Mungu akupe nini,” akatupilia mbali mtindo huo wa maisha na kuachana nayo moja kwa moja. Hivi ndivyo walivyofanya wabatizwa wa zamani, walivua vazi la zamani na kuvishwa vazi jipya lenye rangi nyeupe kuonesha mwanga mpya na maisha mapya katika Kristo Yesu.

Kisha Yesu anamwuliza kipofu: “Wataka nikufanyie nini?” Swali hili linaonekana kama vile halina maana, lakini kumbe, ni la muhimu sana kama alivyowauliza Mitume Yohane na Yakobo waliotegemea utukufu wa ulimwengu huu, aliwauliza “mwataka niwatendee nini?” Kwa vile huwezi kujua kipofu huyu pengine alihitaji kushikwa shavu kidogo au alihitaji chakula au kurushiwa nguo nk. Kwa hiyo, swali lina lengo la kujua kipofu huyu anataka nini hasa toka kwa Yesu. Hilo ndilo swali analoweza kuulizwa kila mmoja wetu: “Unataka nini kwa Yesu. Unataka nini kwa kuwa Mkristo mkatoliki.” Kumbe kipofu huyu alitaka kuwezeshwa. Hebu sikiliza jibu lake: “Mwalimu wangu, nataka nipate kuona.” Neno “kuona” lililotumika hapa kwa Kigiriki ni Anablepso –lenye maana ya kuangalia juu (ana ni juu, na blepo ni kuona). Kipofu huyu anataka kuangalia juu, kwani hadi sasa alikuwa anaangalia chini kwenye mali ya duniani, kwenye utukufu wa ulimwengu huu, kwenye raha na upendeleo wa dunia hii tu.

Yesu akamjibu: “Enenda zako, imani yako imekuponya.” Hakuna hata pahala pamoja katika Injili Yesu anaposema: “mimi nimekuponya,” bali daima anasema: “Imani yako ndiyo imekuponya,” maana yake kazi ya Yesu ni kuonesha mwanga wa kumwezesha kipofu kuzifuata nyayo zake katika njia inayoongoza maisha ya kweli. Kwa hiyo mtu anahitaji kupata mwanga huo na kuamini kwamba, anaweza kuona maisha ya juu.

Endapo unajiona kuwa ni kipofu na unataka kusaidiwa kuona hapo Yesu atakusaidia uweze kuuona mwanga. “Katika mwanga wako tunaona mwanga.” Hatuna budi kuwa na imani na kujiaminisha kwa mwanga wa Neno lake tunalolisikia toka kwa wafuasi wake nasi tutaangazwa. Ukifunguka macho na kupata mwanga huo utaweza kuingia tena barabarani na kutembea sawasawa kama huyu kipofu “Mara akapata kuona; akamfuata njiani.” Anayetaka kuangazwa na Kristo hana budi kufuata mbinu za kipofu huyu, yaani afanye uchaguzi wa kuachana na kijiwe chake halafu kutupilia mbali mgololi, kuinuka na kumfuata Kristo. Hapo upoo! Kazi kwako! Ukitaka unaweza “kula shavu” kutoka kwa Yesu!

Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.