2015-10-20 10:05:00

Ondoeni ubinafsi, litendeeni taifa haki kwa kumchagua kiongozi makini, mwadilifu


Tanzania iko katika kipindi muhimu cha maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Ni wajibu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la uchaguzi, kwa kufuatilia hotuba za kampeni, ili kufikia uamuzi wa busara na kuchagua viongozi wenye sera na sifa za kuliongoza Taifa la Tanzania katika misingi ya amani, umoja, ustawi na maendeleo ya watanzania wote.

Hii ni changamoto pia yak usali ili kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kutambua viongozi watakaofaa kuliongoza taifa la Tanzania. Uamuzi wa kumchagua kiongozi uwe  ni matunda ya sala na maombi, ili kuondokana na ubinafsi, ili kutenda haki pamoja na kufuata dhamiri nyofu. Kila mpiga kura ajiridhishe kuwa anampigia na kushiriki kumchagua mtu anayefaa, mchapakazi, mwadilifu, msema kweli na chachu ya kukoleza maendeleo.

Hii ni sehemu ya Waraka wa kichungaji uliotolewa na Askofu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda ambaye pia ni msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Geita na kusomwa katika majimbo haya mawili, Jumapili tarehe 18 Oktoba 2015, ili kuhamasisha ushiriki wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika mchakato wa uchaguzi mkuu kwa Mwaka 2015.

Watanzania wasipoacha ubinafsi anakaza kusema Askofu Nkwande, watalichagulia taifa viongozi wabovu kwa kusukumwa na “uchama”, udini na ukabila; mambo ambayo ni dhambi. Kiongozi bora si lazima atoke kwenye chama au dini au kabila lako. Hii ndiyo maana waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kufunga, kusali na kuomba, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaonesha kiongozi anayefaa kuliongoza taifa la Tanzania katika awamu ya tano. Watanzania wasipokuwa makini, watachagua kwa kufuata ushabiki na mkumbo, kielelezo cha ubinafsi.

Askofu Nkwande anawataka waamini kuboresha mazingira ya kupiga kura, kwa Mapadre kuweza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumamosi jioni ili kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu. Kwa wale watakaoshindwa kuadhimisha Ibada ya Misa Jumamosi, basi wanaweza kutekeleza wajibu huu kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Jumapili jioni baada ya saa 10 Jioni. Wazee, wanawake na vijana wanashauriwa kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu Jumamosi, tarehe 24 Oktoba 2015 ili kuepuka usumbufu pamoja na kuchelewa kwenda kupiga kura. Hata hivyo Maparoko wameachwa huru kutumia hekima mintarafu mazingira ya kichungaji katika Parokia zao.

Askofu Nkwande anahitimisha Waraka wake wa kichungaji kwa kuwahimiza watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura kuhakikisha kwamba wanatumia haki na wajibu wao Kikatiba kupiga kura bila kufuata ushabiki, misikumo, masilahi binafsi, bali mafao ya watanzania wengi yapewe kipaumbele cha kwanza. Asiwepo mtanzania ambaye ataacha kwenda kupiga kura kwa makusudi. Kila mtu awajibike na kura yake, ili kwa pamoja watanzania waweze kulijenga taifa katika misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.