2015-10-20 10:06:00

Muhtasari wa vikao vya Sinodi kwa siku ya Jumatatu


Jumatatu 19 .10.2015, Wakati wa Mkutano wa kawaida wa Wanahabari kupewa Muhtasari wa Vikao vya Mababa wa Sinodi kwa siku husika, walioshiriki katika kutoa muhtasari huo, pamoja na Padre Federico Lombardi Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Habari ya Vatican, pia walikuwepo wageni waalikwa : Mwenye Heri Patriaki Fouad Twal, wa Upatriaki ya Yerusalemu ya Mashariki, pia Askofu Mkuu  Mark Benedict Coleridge, Askofu Mkuu wa Brisbane Australia na Askofu Solmi Henry, Askofu wa Parma. Msgr. Coleridge  akiwa pia  msemaji wa kundi moja dogo. Na pia Msgr. Solmi hadi hivi karibuni  alikuwa Mkuu wa Tume kwa ajili ya huduma ya kichungaji ya familia kwa Baraza la  Maaskofu la Italia.

Padre Federico Lombardi alikumbusha adhimisho kubwa la Jumamosi iliyopita ambayo ilikuwa kumbukumbu ya kutimia miaka 50 ya Sinodi ambamo kulitolewa nyaraka mbalimbali za majadiliano na maandiko mbalimbali yaliyokwisha fanyiwa kazi na kutolewa tafasiri katika   Kiingereza na Kihispania. Pia kwamba wanasubiri matoleo mengine katika lugha ya kifaransa.

Aidha Padre Federico Lombardi aliwakumbusha wanahabari juu  mwaliko wa Mkesha wa Wadomenican wa Jumanne katika nyumba yao ya Mtakatifu Sabina  kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 800 ya Shirika la Wadomenicani.

Na kwamba kwa kutoka Ukumbi wa Sinodi kwa  Jumatatu asubuhi hapakuwa na michango mipya zaidi. Na hivyo aliwaalika wageni waalikwa kujibu maswali ya wanahabari.  

Patriaki Twal, akiizungumzia mikutano ya Sinodi, alilitaja tukio hili kuwa ni jukwaa linalotafuta  kuweka  yaliyo  mema yote kwa ajili ya  familia. Na pia imekuwa ni ishara nzuri inayoonyesha  umoja wa Maaskofu, licha kwamba wametoka mazingira tofauti, na hivyo kutokuwa na  changamoto sawa. Na pia ni jambo la kawaida kuwa na maoni tofauti katika baadhi ya vipengere na lakini ni wazi hufikia mahali pa wote kukubaliana. Na kwamba katika kazi za wiki mbili zilizopita,  katika kazi ya Sinodi, hapakuwa na kipengere kilichoachwa bila kuguswa kinachohusu hali ya familia duniani kote.  Vikao vilitafuta njia za kuboresha zaidi maisha ya  familia, katika  maana ya  kibinadamu, kidini na kama Kanisa zima.

Na kwa upande wa kupokea Ekaristi kwa wanandoa waliopeana  talaka na kuoa au kuolewa tena, kanisa halina jibu moja la ujumla, lakini kila kesi itatazamwa kipekee na kutolewa jibu  kulingana na mazingira ya tatizo la wanandoa husika. Hili ni suala  nyeti na hivyo haliwezi  kujumlishwa. Ni lazima kutazama kwa makini msingi wa tatizo, pamoja na kuwa na hurumani lazima kuzingatia  mafundisho ya Kanisa.

Na Askofu Mkuu Coleridge, alilenga zaidi katika kukamilika kwa mkutano wa Sinodi akisema kwamba, majadiliano ya Sinodi hii , si kwamba yanafungwa Jumapili ijayo, lakini yataendelea na safari yake  bila ukomo.  Na kwamba upana wa mada zinazojadiliwa, ni moja ya sababu kwa nini  kumekuwa na changamoto nyingi katika majadiliano.

Naye pia alirejea majadiliano juu ya suala la wanandoa wanaopeana talaka na kuoa au kuolewa tena, kwamba inawapasa Maaskofu si kufikiri katika misingi ya kufikirika, lakini  hasa kutazama  vizuri mizizi ya  hali halisi ya tatizo la  kwa kila wanandoa wanaotaka kutalakiana. Na kwamba la muhimu si kuwa na maono ya juu juu matupu, lakini ni lazima kuzingatia uzoefu wa maisha ya binadamu katika taratibu na mapana yake.  

Ni lazima kuwa na mazungumzo ya kweli  ya kina na wanandoa wenye matatizo. Na hivyo kutokana na mazungumzo ya kweli kwa wanandoa husika, hapo inawezekana kutoa maoni ya kuelimisha kulingana na mafundisho ya Kanisa. Alisema  kwamba, Mababa wa Sinodi hawaoni msingi wa  kufanya mabadiliko katika mafundisho ya Kanisa. Askofu Mkuu Coleridge, aliendelea kusisitiza kwamba, ni lazima waliooa au kuolewa tena, kuambiwa ukweli na kwa uwazi zaidi masharti ya kurudi katika  usharika wa Kanisa, kupokea Ekaristi . Ingawa katika baadhi vikundi vya majadiliano ya kazi za Sinodi, baadhi walitaka uwepo wa kitendo cha huruma kwa wanandoa kama hao, Huruma ya  Papa wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya Huruma ya Mungu.  

Na Askofu Solmi ameutaja Mkutano huu wa Sinodi kwamba , umeliwezesha Kanisa kupumua hewa safi ya uzima zaidi kwa Kanisa zima la Ulimwengu.  Mkusanyiko huu wa Maaskofu kutoka pande mbalimbali za Dunia hapa Roma, kujadili masuala ya ndoa na familia katika hali ya uwazi zaidi, masuala yao, matatizo yao, na hata  maadili na mawazo yao kwa pamoja, umekuwa ni wakati nyeti ambao kwa mara nyingi  hasa katika dunia ya nchi za Magharibi ni suala lililokuwa limesahaulika.

Na ameasa kwamba, majadiliano ya Sinodi hii  hayakuwa ya kujipamba kwa "vipodozi”, lakini ni majadiliano ya kina halisi juu ya  Familia kama ni kitovu cha Kanisa na jamii. Kwa mtazamo wa njia Maungamo yaliyopendekezwa kwa wanaopeana talaka  na kuoa au kuolewa tena, Askofu  Solmi, alirudia kutaja umuhimu wa  Kanisa kuongozana na wale walio katika matatizo na zaidi sana wenye kutambua haja ya kuomba msamaha wa  Mungu, wale  wanaopenda kujipatanisha tena na Kanisa lenyewe. Hatimaye, alionyesha matumaini yake kwa matokeo ya Sinodi,  kwamba Sinodi hii imefanyika kwa ufahamu kamili wa umuhimu wa familia kutembea katika njia ya maisha ya Kanisa, wito familia na nafasi yake halali ndani  katika Kanisa.  Na ameonyesha matumaini yake  kwamba, kwa utambuzi huu  hili, inakuwa ni  ishara ya nguvu kwa jamii  na taifa zima .  Alieleza kwa kuzingatia hasa  mazingira Italia,  ambamo mara nyingi  anasema, utaratibu  wa kijamii umesahau misingi ya familia.








All the contents on this site are copyrighted ©.