2015-10-20 08:59:00

Jengeni mazingira ya utulivu na amani, ili uchaguzi mkuu uwe huru na wa haki!


Waamini wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Pwani ya Pembe, Jumapili iliyopita, tarehe 18 Oktoba 2015, wameadhimisha Ibada ya Kiekumene ili kuombea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini huko tarehe 25 Oktoba 2015, ili uweze kuwa wa haki na amani iweze kutawala, ili kutoa fursa kwa wananchi kutekeleza wajibu na haki yao ya Kikatiba kwa kuwachagua viongozi watakaokuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa wananchi wote wa Pwani ya Pembe.

Ibada hii ya Kiekumene imehudhuriwa pia na viongozi wa Serikali na wanasiasa katika ujumla wao, ili kumlilia Mwenyezi Mungu aweze kuwajalia zawadi ya amani na utulivu wakati na baada ya uchaguzi mkuu, kwani chaguzi nyingi zimekuwa ni chanzo cha maafa na mahangaiko ya wananchi wengi Barani Afrika. Ibada hii ya kiekumene imeadhimishwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Parokia ya Agboville na kuongozwa na Askofu Alexis Youlo Touably, Rais wa Baraza la Maaskofu Pwani ya Pembe.

Viongozi wa kidini kwa namna ya pekee wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuomba huruma kwa Mungu kutokana na dhambi mbali mbali ambazo wametendeka kwa kuhatarisha amani, haki, ustawi na mafao ya wengi katika maeneo yao. Wamwombe Mwenyezi Mungu awasamehe na kuwajengea tena uwezo wa kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho, kila mtu katika eneo na mazingira yake ya kazi.

Viongozi wa Kanisa wanawataka wananchi wote kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha mazingira ya haki, amani, ukweli na uwazi wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi nchini Pwani ya Pembe. Kila mwananchi atambue kwamba, ulinzi na usalama ni dhamana anayopaswa kuitekeleza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi na wala si kazi ya vyombo vya ulinzi na usalama peke yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.