2015-10-19 07:23:00

Missio na mkakati wa huduma kwa wakimbizi kutoka Burundi


Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Ujerumani, Missio katika taarifa yake kwa mwaka 2015 linasema kwamba, Tanzania imepokea na kutoa hifadhi kwa wakimbizi zaidi ya laki  moja na nusu kutoka Burundi kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo kwa sasa. Tanzania imepewa kipaumbele cha kwanza katika msaada unaotolewa na Missio sehemu mbali mbali za dunia, ili kuweza kutoa hifadhi kwa wakimbizi wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha nchini Tanzania.

Taarifa ya Missio inaendelea kusema kwamba, lengo ni kuliwezesha Kanisa nchini Tanzania kuonesha upendo na ukarimu kwa wakimbizi na kwamba, sadaka na majitoleo yote yaliyokusanywa tarehe 9 na 11 Oktoba, Siku maalum za kuhamasisha ari na mwamko wa kimissionari nchini Ujerumani, yatatumika kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wanaohifadhiwa nchini Tanzania.

Viongozi wa Kanisa kutoka Tanzania wameshiriki katika maadhimisho haya, ili kuonesha mchango wa Kanisa katika kuwahudumia wakimbizi wanaolazimika kuikimbia nchi yao kutokana na machafuko ya kisiasa yanayojikita katika uchu wa mali na madaraka, pasi na kuzingatia haki, amani na mafao ya wengi. Hii imekuwa pia ni fursa kwa viongozi wa Kanisa kuonesha mchango wa Kanisa nchini Tanzania katika sekta ya afya, elimu na huduma za kijamii; mambo yanayojikita pia katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene.

Missio katika kipindi cha mwaka 2014 imetumia kiasi cha Euro millioni 49 ili kugharimia miradi 850 iliyotekelezwa Barani Afrika, Asia na Oceania. Malengo ya mwaka 2014 na mwaka 2015 ni kusaidia mchakato wa kutengeneza fursa za ajira kwenye kambi za wakimbizi, ili kuwajengea uwezo wa kuzitegemeza familia zao. Missio inatarajia kuongeza kiasi cha fedha kwa wakimbizi ifikapo mwaka 2016.

Kanisa Katoliki kwa sasa liko mstari wa mbele katika mchakato wa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaoteseka kwa kunyanyaswa na kubaguliwa kutokana na sera zisizojali utu na heshima ya binadamu. Monsinyo Klaus Kràmer, Rais wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Ujerumani, Missio anasema, kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi, Kanisa linajikuta kwamba, linakabiliwa na hali ngumu kiasi cha kufanya kazi kupita uwezo wake.

Kiasi cha Euro millioni 2.6 kimetumika kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria na Iraq. Missio inakiri kwamba, mchango wa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kwa mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 5% ikilinganishwa na miaka mingine. Hii ni sawa na ongezeko la Euro millioni 20. Katika maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani kwa mwaka 2014, waamini walichanga kiasi cha Euro millioni 4, fedha ambayo imetumika kwa ajili ya kugharimia miradi ya shughuli za kichungaji na maendeleo Barani Afrika, Asia na Oceania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.