2015-10-18 08:23:00

Hija ya pamoja katika kipindi cha Miaka 50! Si haba! Matunda yanaonekana


Ilikuwa ni tarehe 15 Septemba 1965, Mwenyeheri Paulo VI alipoanzisha rasmi maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu na tangu wakati huo, Kanisa limeadhimisha Sinodi za Maaskofu 27, kama sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa wa kutaka kuimarisha imani na matumaini miongoni mwa watoto wake. Wakleri na malezi yao; haki na amani; Uinjilishaji na Katekesi; toba na upatanisho; wito na utume wa waamini walei; maisha ya kuwekwa wakfu; utume wa Maaskofu katika shughuli za kichungaji; Ekaristi Takatifu na Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na Familia. Hizi ni kati ya mada ambazo zimechambuliwa na Mama Kanisa katika kipindi cha miaka hamsini tangu kuanzisha kwa Sinodi za Maaskofu.

Hii ni sehemu ya muhtasari uliotolewa Jumamosi tarehe 17 Oktoba 2015 na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu wakati wa kilele cha Jubilei ya miaka 50 ya Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu. Maadhimisho haya yameimarisha umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu mahalia na kwamba, Sinodi zimekuwa ni chombo makini cha utekelezaji wa maazimio na changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita. Matunda ya maadhimisho hayana yanaendelea kujionesha katika maisha na utume wa Kanisa, sanjari na huduma kwa familia ya Mungu katika ujumla wake.

Kardinali Baldisseri anasema, Sinodi za Maaskofu kimekuwa ni chombo cha majadiliano ya Kanisa na walimwengu katika misingi ya ukweli na uwazi, kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu. Huu ni mchakato unaopania kuleta wongofu na mabadiliko katika shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa, daima akijitahidi kusoma alama za nyakati, tayari kutoka kimasomaso kwa ajili ya Uinjilishaji mpya. Sinodi ni chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni chombo kinachotekeleza dhamana na wajibu wake kwa kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mama Kanisa katika kipindi cha miaka hamsini ya Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, ametoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa familia. Kuna Sinodi tatu ambazo zimejikita katika tafakari ya familia na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo, ili kuliwezesha Kanisa kufanya mageuzi na kuendelea kuwa aminifu kwa Injili ya Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.