2015-10-17 06:59:00

Usitafute ujiko, bali utumishi na mafao ya wengi!


Ni jambo la kawaida kumwona mwanafunzi akihangaika kupata ufanisi katika masomo yake. Na pale anapofikia utimilifu wa juhudi ya kazi yake furaha umtembelea na huyo uonesha kila namna ya kuwa na hali ya kuridhika. Kwa bahati mbaya wengi wao ufanisi huo wanauona zaidi katika ufaulu wa mitihani yao. Hali kama hiyo pia inaweza kuwepo katika juhudi zetu za kuishika imani yetu. Kila mmoja anajaribu kuielewa kwa makusudi ya kufikia utimilifu wake. Mmoja atajitahidi kufuata sheria mbalimbali na taratibu mahalia ili asiingie katika kundi la wale wanaoweza kuonekana watovu wa nidhamu na watendao mambo maovu. Lakini changamoto inakuja leo hii mbele yetu kila mmoja, kutafakari juu ya ufuasi wetu. Ni nini kinatusukuma kufanya haya? Je, tunatafuta utumishi au ujiko? Je, ufuasi wetu ni kwa ajili ya kupewa tuzo mbinguni au ni kwa ajili ya kutufanya tukue na kuufikia ukamilifu wa wana Mungu?

Injili ya leo inatupatia mwanga wa namna ya kupata suluhisho kwa changamoto tulizojipatia hapo juu. Kristo anatuambia katika somo la Injili: “Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote”. Mwanzoni mwa Injili ndugu wawili waana wa Zebedayo, Yakobo na Yohana wanatafuta upendeleo wa kuwa karibu na Yesu katika Ufalme wa mbinguni. Wanafikia hata kudiriki kujiaminisha kwamba wapo tayari kupitia njia yoyote ili mradi tu kupokea hiyo tuzo. Kwa maneno mengine ufuasi wao unatiwa motisha na tuzo watakayoipokea. Si kuangalia maana ya ufuasi wao bali ni kuangalia kile ambacho watapokea mwishoni, kuwa karibu kabisa na Kristo: “utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto katika ufalme wako”.  

Ukristo unatudai kwa nafasi ya kwanza utumishi. Imani yetu tunayoipokea kama tunu inatudai na sisi kuitoa kwa wengine kama tunu. Kila mmoja anapaswa kujiona anapasika kujitoa kikamilifu na kutumikia wenzake. Amri na taratibu tunazopewa si kwa ajili ya kupewa tuzo au kupata sifa fulani. Nyenzo hizi zinapaswa kuwa  njia ya kutufanya tukue zaidi kiimani na kiutu. Kwa maneno mengine zinatufanya tuurithi ufalme wa mbinguni au tunafanywa kuketi kuume au kushoto kwa Kristo katika mazingira yetu ya kawaida. “Utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa”.

Kristo anaonekana katika wenzetu tunaoishi nao na kwa namna ya pekee wahitaji. Huko ndipo kuna nafasi za kukaa upande wa kuume na kushoto mwa Kristo. Hiyo ndiyo tunu tuliyowekewa na ambayo tutaifikia kwa kuwa tayari katika utumishi. Tunakumbushwa katika dominika hii kuutumia ukristo wetu sio kama ngazi ya kupokea tuzo au kufikia mbinguni bali imani yetu itufanye tuendelee kukua siku hadi siku katika tunu mbalimbali za kikristo na katika utu wetu.  

Pia tunahimizwa na Injili hii kuepa kutenda jambo fulani liwe la kiimani au la kijamii kwa kunuia tuzo bali tutende kwa sababu tunastahili kutenda na ndivyo ilivyopaswa kutenda. Tunaalikwa kutenda kwa sababu ndiyo wajibu wetu kutokana na nafasi mtu aliyo nayo hivyo kwa manufaa ya wote. Tunapoingia katika mtego wa kutenda kwa sababu ya kukuza jina lako au kupata sifa fulani fulani za kibinadamu ndipo tunapojikuta tunaingia katika matendo ya kutotenda haki kwa wengine, kutokuwa watu wa haki, kuwa wabadhirifu wa mali za umma na mengine yanayochukiza katika nafasi za utumishi. Inatosha tu kutafakari wale ambao wanawania nafasi mbalimbali za uongozi iwe ni katika siasa, makazini au katika jamii ndogo. Wale ambao wanatafuta jina na ukubwa huishia kuwa mabwana, yaani, wale wanaokuwa juu ya wengine na kuwatumikisha. Watu wa namna hii huishia kuwa wabadhirifu, wanyonyaji na wanaowanyanyasa wengine. Watatumia njia nyingi za rushwa ili mradi tu kurejea katika nafasi zao na kuendelea kuwafanya wale walio chini yao wanalambe vumbi tu.

Somo la pili la dominika hii linamweka Kristo kuhani wetu mkuu  na kwa namna nyingine katika somo la kwanza, Yeye anaonekana katika sura ya Mtumishi mwenye haki  na anawekwa mbele yetu kama dira yetu. Yeye aliye Mungu anakuja kwetu katika hali utumishi akiwa amejivika unyenyekevu. Mwandishi wa barua kwa Waebrania anatuambia kwamba: “hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi”. Na pia Nabii Isaya anakazia wazo hilo akisema: “Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki; naye atayachukua maovu yao”.

Kwa unyenyekevu mkubwa hivi Kristo anatufundisha namna njema ya kutumikia, yaani, kushuka chini na kuivaa hali ya unaowatumikia na kwenda nao katika ufanisi. Hapa, juhudi hii ya kujenga ufalme wa Mungu au kutafuta hizo nafasi za kuume au kushoto kwa Krsito inaelekezwa tena katika maisha na mazingira yetu ya kawaida.  Mtumishi huyu mwenye haki anayezungumziwa na Nabii Isaya ni Kristo ambaye katika hali ya unyenyekevu anashuka chini na kuvaa ubinadamu wetu na kujitwika dhambi zetu kusudi mimi na wewe tuokolewe. Kuujenga ufalme wa Mungu ni kuishi na yule Kristo ambaye anaonekana katika sura ya mwitaji anayejitokeza mbele yako. Hivyo basi utumishi wetu unazidi kuhimizwa kujikita katika kuustawisha ufalme wa Mungu na kuwafanya watu wote wauone utukufu wa Mungu.

Katika Dominika hii ya 29 ya Mwaka B Mama Kanisa pia anadhimisha siku ya themanini na tisa ya umisionari duniani. Katika ujumbe wake kwa mwaka huu ambapo pia Kanisa lipo katika maadhimisho ya mwaka wa maisha ya wakfu Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, “kuna uhusiano wa pekee kati ya maisha ya kitawa na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika ufuasi kwa Kristo Yesu, chemchemi ya maisha ya kitawa. Watawa wanaalikwa kwa namna ya pekee, kubeba vyema Misalaba yao, tayari kumfuasa Kristo, ili kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Watu wa Mungu, kwani uwepo wa Kristo unachapa ya kimissionari na kwamba, hii pia ni sehemu ya maisha ya kitawa na vinasaba vyake”.

Tuombe katika dominika hii neema ya Mungu kusudi itusaidie kuendelea kukua na kuimarika katika ufuasi wetu. Roho Mtakatifu atuangazie katika kulielewa Neno la Mungu na Mwili na Damu Takatifu ya Kristo vitutie nguvu kusudi tupate ujasiri wa kujivua vilema hivyo vya kutafuta ukubwa na mwishowe tuwe tayari kumtumikia Kristo na kuutafuta Ufalme wake katika utumishi wetu kwa wale wanaotuzunguka na kwa namna ya pekee, wale walio na uhitaji mkubwa wa upendo wetu wa kikristo.

Na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.