2015-10-17 15:00:00

Matunda ya Jubilei ya miaka 50 ya Sinodi za Maaskofu!


Mababa wa Sinodi katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Sinodi za Maaskofu wamepata fursa ya kushirikisha mchango wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa na Makanisa mahalia, kwa kumshukuru Mwenyeheri Paulo VI aliyekuwa na mwono wa Kinabii, changamoto kutoka kwa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kardinali Soane Patita P. Mafi, ambaye niRais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Pacific, anashukuru sana mchango wa Sinodi za Maaskofu ambao umesaidia kuunda Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Katoliki Oceania, muungano wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka Pacific.

Shirikisho hili limekuwa ni kielelezo makini cha umoja na mshikamano wa Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu, kwani maadhimisho ya Sinodi imekuwa ni fursa kwa Maaskofu kukutana, kusali na kutafakari kwa pamoja changamoto za maisha na utume wa Kanisa, licha ya fursa, matatizo na changamoto zinazojitokeza katika maadhimisho haya. Nyaraka mbali mbali zilizotolewa na Mapapa katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, zimekuwa ni nyaraka rejea katika utekelezaji wa mikakati na shughuli za kichungaji kwa Makanisa mahalia, kwa kuwa na dira, mwelekeo na miongozo mbali mbali, inayoonesha umoja na mshikamano wa Kanisa.

Makanisa mahalia yameweza pia kuadhimisha Sinodi, kwa kuangalia vipaumbele vya Makanisa yao, hususan katika: azma ya Uinjilishaji mpya pamoja; kuendelea kusoma alama za nyakati pamoja na dhamana na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa. Sinodi zimewasaidia waamini kujiwekea sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, katika umoja na mshikamano, huku wote wakitembea kwa pamoja. Waamini kutoka Oceania wanaendelea kusali kwa ajili ya kuombea maadhimisho ya Sinodi ya  familia, kwani familia ni kiini cha maisha ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Naye Patriaki Louis Raphael Sako wa Kanisa la Wacaldei wa Babilonia anasema, Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu umelitajirisha Kanisa kwa kuwapatia Maaskofu fursa ya kujadiliana kwa pamoja wanapotekeleza sauti yao ya kinabii, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kwa ajili ya mafao ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake kwa kujikita katika: maisha, taalimungu, tasaufi, shughuli za kichungaji, utume na nidhamu.

Huu ni mchakato wa malezi unaojikita katika kuhabarisha na kutembea pamoja, changamoto kwa Mabaraza ya Maaskofu kushirikiana na kushikamana kwa pamoja. Nyaraka na ujumbe kutoka kwa Mababa wa Sinodi zimekuwa na mafao makubwa kwa familia ya Mungu, kwa kuonesha ujasiri na umoja. Makanisa yenye rasilimali watu na fedha kidogo yasaidiwe ili yaweze pia kuadhimisha Sinodi kwa ajili ya maeneo yao, ili kukuza ari na mwamko wa Kiinjili pamoja na kusoma alama za nyakati.

Kwa upande wake Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales amegusia umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu katika maisha na utume wa Kanisa Barani Ulaya, kwa kuonesha umoja na mshikamano wa Kanisa hususan baada ya kinzani na misuguano ya Vita kuu ya Pili ya Dunia; mchango wa Wamissionari kutoka Ulaya katika mchakato wa Uinjilishaji wa Awali sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kuendelea kushirikisha tunu msingi za Kiinjili na utajiri wa Mapokeo ya Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi yamekuwa ni fursa ya kuwakutanisha Maaskofu mbali mbali ambao wametoa mchango mkubwa katika maisha ya Familia ya Mungu.

Imekuwa ni nafasi ya kuimarisha majadiliano ya kiekumene na umoja wa Kanisa; Uinjilishaji mpya kwa kukumbatia tunu msingi za Kiinjili, maadili na utu wema, unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Sinodi zimekuwa ni chachu ya utamadunisho wa Kiinjili ndani na nje ya Bara la Ulaya. Kinzani na hali ya kutoelewana ni mambo yaliyojitokeza, lakini Kanisa linazidi kuchanja mbuga! Umwilishaji wa baadhi ya nyaraka za Sinodi, mahusiano kati ya Kanisa na vyombo vya habari; mtindo na mfumo wa kuwashirikisha waamini katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu ni kati ya changamoto pevu zinazopaswa kufanyiwa kazi ili kupata ufanisi mkubwa zaidi.

Wakati huo huo, Kardinali Christoph Schònborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna anasema, iliwachukua Mababa wa Kanisa takribani miaka 450 tangu kuadhimishwa Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu ili kuanzisha Sinodi za Maaskofu, changamoto kutoka kwa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba, maadhimisho ya Sinodi ni fursa makini katika utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Mbinu za maadhimisho ya Sinodi imefanyiwa marekebisho makubwa na Papa Mstaafu Benedikto XVI pamoja na Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuzipatia mwelekeo wa kitaalimungu na kisheria; mambo yanayopaswa bado kuendelea kuboreshwa. Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu uwe ni kielelezo na mfano wa kuigwa katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu. Sinodi zinaweza kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa maisha na utume wa Kanisa; kielelezo cha ushuhuda wa umoja na mshikamano wa Kikanisa. Ni mahali pa kufanya mang’amuzi ya pamoja kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa, kwa kukuza na kudumisha ari ya kimissionari sanjari na kukomaza huduma ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.