2015-10-17 12:09:00

Jubilei ya huruma ya Mungu ikuze majadiliano ili kuondoa vita na kinzani!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu tunakusalimu kwa mara nyingine tena kutoka hapa Radio Vatican, Tumsifu Yesu Kristo! Karibu tuendelee kuupitia waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu; si waraka mwingine bali ni ule ule maarufu kwa jina la ‘Misericordiae Vultus’ yaani Uso wa Huruma.

Katika kipindi hiki tunaona jinsi Baba Mtakatifu anavyoionesha Huruma ya Mungu kama amana kwa watu wote. Huruma ya Mungu haifungwi tu katika mipaka ya Kanisa, bali huiendea familia nzima ya mwanadamu. Ni kwa mantinki hiyo, tunafundishwa kwamba “huruma ya Mungu baba, huwainua wote, huwafariji wote, huwatakasa wote na mwisho wote waokolewa kwayo”.

Ni mwito kwetu sote kutakiana huruma ya Mungu, kuombeana huruma ya Mungu, na zaidi tena tufurahishwe sana pale ambapo tunaonja kuwa jirani zetu wametembelewa na huruma Mungu. Na zaidi sana, tuwe tayari kuwa vyombo vya huruma ya Mungu, ili kuweza kupeleka huruma ya Mungu kwa wenzetu bila kujali walizaliwa wapi, wana rangi gani, wanaamini nini au wanakula nini. Huruma ya Mungu wetu ni kwa ajili yetu sisi sote. Jinsi tunavyojibidisha kupeleka huruma ya Mungu kwa watu, ndivyo nasi wenyewe tunavyohurumiwa zaidi na zaidi, na ndivyo tunavyozidi kuonja furaha ile ya huruma ya Mungu.

Kwa mtazamo huo Baba Mtakatifu Francisko anasema, “kuna dhana ya huruma, inayoenda ng’ambo ya mipaka ya Kanisa’. Hata katika dini za Kiyahudi na Kiislamu, huruma inatazamwa kama mmoja na sifa muhimu sana ya Mungu. Israeli alikuwa wa kwanza kupokea ufunuo huu, ambao unaendelea katika historia kama chanzo cha utajiri na wema usiokoma, uliotolewa ili kuweza kuwashirikisha wanadamu wote”. Kama tulivyokwisha kuona, Agano la Kale limejengwa zaidi katika huruma ya Mungu. Agano hilo linasimulia kazi ya Mungu aliyoifanya kwa watu wake wakati wakiwa katika magumu mbalimbali ya historia yao. Daima Mungu alitenda makuu kati yao kwa kuwa huruma yake ya dumu milele.

Na katika dini ya Kiislamu, dhana ya Mungu mwenye huruma ni kati ya tunu msingi. Kati ya majina ambayo Dini yaKkiislamu humwita Mungu ni “Rahimu na Karimu”, kumaanisha ‘Mwenye rehema na mwingi wa fadhili au mkarimu’. Aina hii ya sala  daima imo midomoni mwa waamini Waislamu, ambao kweli hujisikia kuwa wakisindikizwa na kusaidiwa na Mungu mwenye huruma, anayewaonea huruma katika madhaifu yao ya kila siku, na Mungu mkaribu anayewasaidia katika maitaji ya maisha yao. Kwa sala hiyo, wanapata nguvu ya kuendelea kumwangukia huku wakimwabudu na kumlilia katika dhiki zao. Nao pia huamini kwa dhati kwamba, hakuna anayeweza kuiwekea mipaka huruma ya Mungu,  kwa sababu milango yake daima iko wazi kwa wote.

Baba Mtakatifu anaongeza kusema “ninaamini kwamba mwaka huu wa Jubilei, ambapo tunaiadhimisha huruma ya Mungu, utachochea makutano kati ya dini hizi na mapokeo ya dini nyinginezo. Na tena Mwaka huo wa Huruma ya Mungu ufungue mijadala zaidi ili tuweze kuelewana na kutambuana vema zaidi. Mwaka huo wa Jubilei, uondoe kila aina ya ufinyu wa fikra mintarafu imani za watu. Mwaka huo wa huruma ya Mungu, uondoke kila aina ya kubaguana na kunyanyasana kwa kigezo cha imani. Mwaka huo uondoe kila aina ya kutoheshimiana, na ufukuzie mbali kila aina ya fujo na utengano”.

Baba Mtakatifu anaendelea kuupamba Mwaka huo Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu kwa kuyaelekeza mawazo yake wa Mama Bikira Maria, Mama wa huruma kama tunavyomsifu katika Litania ya sifa zake. Baba Mtakatifu anasali kwa Mama Bikira Maria ili upole na tunza yake ya kimama  itulinde katika Mwaka huo Mtakatifu, ili sisi sote tuweze kung’amua furaha ya wema na upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema, “hakuna aliyeweza kuzama katika undani wa Fumbo la umwilisho kama Mama Bikira Maria. Maisha yake yote yaliratibishwa kwa uwepo wa huruma iliyo mwilishwa”. Mama wa yule aliyesulibiwa na akafufuka, ameingia katika madhabahu ya huruma ya Mungu  kwa sababu  alishikiriki kikamilifu katika fumbo la upendo wake.

Kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mama wa Mwana wa Mungu, tangu mwanzo, kwa pendo la Mungu Maria aliandaliwa kuwa Sanduku la agano kati ya Mungu na Mwanadamu. Aliiweka huruma ya Mungu katika moyo wake katika muungano kamili na mwanae Yesu Kristo.  Utenzi wake wa sifa aliouimba akiwa nyumbani kwa Elizabeti, ulielekezwa zaidi kwa huruma ya Mungu ambayo hudumu kizazi hata kizazi (Lk. 1:50).

Baba Mtakatifu anasema, nasi pia tulijumuishwa katika maneno hayo ya kinabii ya Bikira Maria. Haya yatakuwa kwetu ni  chemchemi ya faraja na nguvu; hasa tuwapo katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu, tunapotazamia kuonjeshwa zaidi matunda ya huruma ya Mungu. Tufungue mioyo yetu ili nasi tufanywe kuwa hazina za huruma ya Mungu. Tusikilizate tena kipindi kijacho.

Kutoka katika studio za Radio Vatican, ni mimi Pd. Pambo Martini Mkorwe. OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.