2015-10-16 14:57:00

Zambia: Jumapili tarehe 18 Oktoba 2015: Siku ya kufunga, kusali na toba!


Rais Edgar Chagwa Lungu wa Zambia anawaalika wananchi wote wa Zambia, tarehe 18 Oktoba 2015 kufunga, kusali na kufanya toba ili kuombea ustawi na maendeleo ya wananchi wa Zambia. Huu ni mwendelezo wa Ibada iliyoanzishwa na waasisi wa Zambia kunako mwaka 1964, kwa kuiweka nchi yao chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, ili waweze kujikita katika misingi ya haki, ukweli, upendo kama sehemu ya mchakato wa kukoleza mafungamano, umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa.

Lengo ni kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi ya pekee katika maisha ya wananchi wa Zambia, kila mtu kadiri ya dini na imani yake anasema Rais Lungu. Waamini wamlilie na kumwomba Mwenyezi Mungu ili kuingilia kati na hatimaye, kuyapatia matatizo na changamoto zinazoikumba Zambia: kisiasa, kijamii na kiuchumu majibu muafaka. Anasema, leo hii Zambia imejikuta njia panda kwa kutowaheshimu wala kuwathamini wazee, kukosa uzalendo na heshima; kiwango kikubwa cha watu wasiokuwa na fursa za ajira.

Rais Lungu anasema kuanguka kwa sarafu ya Zambia kumesababisha madhara makubwa katika uchumi wa taifa; ukosefu wa uhakika wa umeme kutokana na ukame wa muda mrefu ambao umesababisha mgawo mkali wa umeme na athari zake zinajionesha katika uzalishaji na utoaji wa huduma kwa wananchi sanjari na kushuka kwa tija na mapato. Wananchi wengi wa Zambia kwa sasa wamekumbwa na msongo wa mawazo na hali ya kukata tamaa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.