2015-10-16 10:18:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Chakula Duniani, 2015


Hifadhi ya kijamii na kilimo ni muhimu katika kupambana na umaskini vijijini, ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 70 ya Chakula Duniani inayoratibiwa kwa namna ya pekee na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO. Licha ya sera na mikakati mbali mbali iliyowahi kufanywa na Jumuiya ya Kimataifa katika ngazi mbali mbali, lakini bado baa la njaa na utapiamlo wa kutisha vinamwanadama mwanadamu kutokana na ukosefu wa usawa katika mgawanyo wa rasilimali ya dunia; uchu wa faida kubwa, mafao binafsi na siasa tenge zinazokwamisha ushirikiano wa Jumuiya ya kimataifa katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani.

Kutokana na mwelekeo huu, uhakika wa usalama wa chakula ni lengo ambalo litakuwa ni vigumu kufikiwa, hata kama FAO inajitahidi kutafuta ufumbuzi wa changamoto hii. Bado nchi nyingi hazijaonesha utashi wa ushirikiano; kuna kinzani na migogoro, madeni makubwa, ukosefu wa huduma za afya na elimu mambo muhimu katika kuwasha moto wa matumaini miongoni mwa jamii. Kuna idadi kubwa ya watu hawana hifadhi za kijamii na kwamba, wanaishi katika umaskini wa hali na kipato na kuwa, mahitaji yao msingi yanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi katika kiwango cha chini kabisa. Wakulima wadogo wadogo wanakabaliana na matatizo kwani wengi wao wanategemea hali ya hewa, wanatumia pembejeo duni, hawana soko la uhakika wa mazao yao na kwamba, miundo mbinu ya barabara na hifadhi ya mazao ya kilimo bado ni duni.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa  Professa Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa FAO katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2015. Changamoto zote hizi anasema Baba Mtakatifu zinaathari kubwa kwa familia, changamoto ya kujenga na kuimarisha mshikamano wa kimataifa, kwa ajili ya mafao ya wengi sanjari na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika kwa ajili ya maendeleo ya wengi. Hiki ni kielelezo cha haki jamii, inayowawezesha wananchi kushiriki katika mchakato wa kufanya maamuzi ya kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Watu wasiokuwa na hifadhi za kijamii wanaathirika sana na majanga asilia na hivyo kuwapoka wananchi matumaini ya maisha bora kwa siku za usoni. Ili kuwalisha wenye njaa kuna haja ya: kujikita katika mshikamano wa kimataifa, kwa kudhibiti athari za kijamii na kiuchumi; majanga asilia, ili kujenga dhana ya usawa kiuchumi, kielelezo cha upendo wa kijamii, ufunguo wa maendeleo ya kweli ya binadamu. Rasimali ya dunia na utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote ni mambo yanayopaswa kutiliwa mkazo, ili kuzienzi familia zinazokabiliwa na changamoto za maisha, kwa kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi, kwa kutoa huduma makini kwa wazee pamoja na kuwaelimisha vijana wa kizazi kipya kwa kuwapatia elimu makini, tayari kushindana katika ulimwengu wa ajira.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa halina majibu ya kisayansi katika utatuzi wa matatizo na changamoto zote hizi, lakini ni mtaalam wa hali hizi. Mazingira na rasilimali ya dunia ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; ambao pia wanapaswa kuwa ni walinzi na watumiaji bora, wanaoshirikiana vyema na wengine. Hii ni changamoto pia ya kusimama kidete kupinga ukosefu wa haki msingi za kijamii, kwa kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Ajenda ya Maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 isiwe ni sheria na mikataba mizuri ya kimataifa isiyotekelezeka, bali ilete mabadiliko ya kweli kitaifa na kimataifa, kwa kuheshimu utu wa binadamu, uhai pamoja na kujikita katika usawa. Kila mtu atekeleze dhamana na wajibu wake kadiri ya nafasi na uwezekano uliopo. FAO itaweza kutekeleza dhamana yake, ikiwa kama itawezeshwa kupata nyenzo muhimu ili kuwahakikisha kwamba, kunakuwepo na hifadhi ya kijamii mintarafu mchakato wa maendeleo endelevu hususani kwa wakulima, wafugaji na wavuvi vijijini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.