2015-10-16 15:10:00

Mwaka wa Watawa Duniani: Iweni mashuhuda wa: Imani, Umoja, Upendo na Maadili


Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa kitawa, unaojikita katika ushuhuda wa Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Maisha ya kitawa yanapaswa kuwa ni shule ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati na chemi ya furaha ya kweli katika maisha. Huu ni mwaliko wa kutafakari na kujitahidi kuiga tunu msingi za maisha ya Mtakatifu Theresa wa Avila, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya miaka mia tano tangu alipozaliwa. Ni mwanamke wa shoka aliyeyakita maisha yake katika tasaufi, iliyoleta mageuzi makubwa ndani ya Kanisa.

Kwa muhtasari haya ndiyo mawazo makuu yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watawa wanaofanya kazi katika Sektretarieti ya Vatican, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na viongozi wakuu kutoka Sekretarieti ya Vatican. Itakumbukwa kwamba, kuna watawa 51 kati yao watawa wa kike ni 31 na wa kiume 20.

Fumbo la Ekaristi Takatifu linaloadhimishwa na kuabudiwa na watawa kama sehemu ya maisha yao ya kila siku ni chanzo na kilele shughuli zao za kitume na kichungaji, kielelezo na ushuhuda wa Sadaka ya Kristo Msalabani. Ekaristi ni chemchemi ya umoja unaopaswa kujionesha katika maisha ya mtawa binafsi, Jumuiya za kitawa na ndani ya Kanisa katika ujumla wake. Lengo ni kushuhudia umoja, upendo na mshikamano dhidi ya vita, kinzani na migogoro inayojionesha sehemu mbali mbali za duniani.

Umoja na mshikamano upewe kipaumbele cha pekee na watawa wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwenye Sekretarieti ya Vatican. Wawe makini ili wasimezwe na "magonjwa ya wafanyakazi wa Vatican” yaliyotajwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni ubinafsi unaokausha ukweli, uwazi na mahusiano ya kibinadamu; kwa kutoshirikisha wengine karama, ujuzi na weledi ambao mtu amekirimiwa katika maisha yake wala kuwa tayari kuwajibika anapokabidhiwa utume wa kutekeleza.

Wafanyakazi wa Vatican wanapaswa kujenga mazingira yatakayokuza na kudumisha umoja na mshikamano kama familia. Sekretarieti ya Vatican iwe ni nyumba na shule ya umoja, ili kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Watawa wawe ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini kwa watu wanaowazunguka na kwamba, Kanisa halipendi kuwaona Watawa wasiokuwa na furaha, kwani furaha ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha uzuri wa Injili na ufuasi kwa Kristo Yesu.

Kardinali Parolin, anawaalika watawa na wafanyakazi wote wa Vatican kusoma na kutafakari maisha ya Mtakatifu Theresa wa Avila, mwanamke wa shoka aliyejikita katika tasaufi na sala kiasi cha kuleta mageuzi makubwa ndani ya Kanisa, leo hii Kanisa linamheshimu kama Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Daima watawa wawe na mwono wa kukazia mambo msingi katika maisha, wanapoendelea kutoa huduma kwa kumzunguka Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Pamoja na kazi, watawa wawe na nafasi ya kushughulikia maisha yao ya kiroho pamoja na kujipatia mapumziko ya kutosha, ili kuwa na nguvu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini. Watawa wawe ni mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu, kwa njia ya matendo, tayari kuwa ni vyombo vya umoja na mshikamano wa dhati, mashuhuda wa furaha na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.