2015-10-16 14:41:00

Mshikamano wa upendo na maskini wa Roma!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 15 Oktoba 2015 mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maskofu, huku akiambatana na viongozi wakuu wa Shirika la Wayesuit, Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta na viongozi waandamizi kutoka Vatican, alitembelea na kukagua Bweni maalum lililozinduliwa hivi karibuni kwa ajili ya kutoa hifadhi ya malazi kwa baadhi ya maskini wa Roma, ambao wengi wao wamekuwa wakilala kwenye viambaza vya nyumba za watu.

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, kwani hawa ndio walengwa wakuu wa Injili inayomwilishwa katika ushuhuda wa upendo. Baba Mtakatifu pamoja na ujumbe wake, walipata nafasi ya kuzungumza na kubadilisha mawazo na maskini wanaotunzwa katika Bweni hili, akaonesha ile Injili ya furaha kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jengo hili ambalo lina uwezo wa kutoa hifadhi kwa watu 34, inahudumiwa na Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta.

Karibu na Vatican kuna “Nyumba zawadi ya Maria” inayotoa hifadhi kwa wanawake 50 wasiokuwa na malazi mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa namna ya pekee, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha katika maisha yao matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.