2015-10-16 15:29:00

Jiepusheni na virusi pamoja na chachu ya unafiki!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake Ijumaa, 16 Oktoba 2015 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican amewataka waamini kuwa macho dhidi ya Virusi vya chachu ya unafiki wanayoweza kuambukizwa. Hii ni changamoto iliyotolewa na Yesu kwa wanafunzi wake dhidi ya chachu ya unafiki wa Mafarisayo kama anavyosimulia Mwinjili Luka.

Yesu alikuwa anawaangalisha wafunzi wake dhidi ya Virusi vya unafiki ili wasiambukizwe kutoka kwa Mafarisayo. Unafiki wa Mafarisayo ni kitu kidogo, lakini madhara yake ni makubwa katika jamii. Unafiki ni hali ya maisha ambayo haioneshi uhalisia wa mambo. Ni hali inayomwonesha mtu kuwa na utulivu na amani ya ndani, lakini kumbe ni kinyume chake, ni sawa na nyoka mwenye sumu. Wanafiki ni watu wanaojiamini kipumbaji, watu wenye majivuno, wanaotaka kutazamwa na watu ili waonekane kuwa ni watu wa maana ndani ya jamii.

Katika mazingira na hali kama hii, Yesu anapenda kuwahakikishia Mitume wake kwamba, hawana sababu ya kuogopa, kwani yaliyofichwa yatafunuliwa na kuanikwa hadharani. Hii inatokana na ukweli kwamba, chachu ya unafiki inawafanya watu kupenda giza badala ya kutembea katika mwanga. Hivi Virusi vinavyosababisha maafa makubwa. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, wanayo thamani kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanaye Mwenyezi Mungu anayewapenda, anayewathamini na kuwatunza.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu anawaonesha wafuasi wake njia muafaka ya kupambana na chachu pamoja na Virusi vya unafiki kwa kusali ili kutokutumbukizwa katika chachu hii ambayo ni hatari sana kwa maisha ya mwamini na kwamba, Sala katika njia yao itawafanulia mwanga wa Mungu. Waamini wanapaswa kusali daima, ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kulilinda na kulisimamia Kanisa na Watu wake, ili wapende mwanga unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili waweze kuwa imara katika njia zao. Awalinde watu wake, ili waweze kutambua kwamba, kuna Mungu anayewalinda na kuwapenda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.