2015-10-15 15:16:00

Sinodi inapania kujenga matumaini katika maisha ya ndoa na familia


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican wakati akiwajuza waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, Jumatano tarehe 14 Oktoba 2015 anakaza kusema, Mababa wanaendelea bado kusikiliza taarifa za makundi madogo madogo pamoja na mchango binafsi kutoka kwa Mababa wa Sinodi. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mababa wa Sinodi kusonga mbele na maadhimisho ya Sinodi katika ukweli na uhuru, kwa ajili ya ustawi wa familia ya binadamu.

Padre Lombardi anasema, si kazi yake kufafanua kwa kina na mapana msamaha ambao Baba Mtakatifu Francisko ameomba kwa Familia ya Mungu kwa niaba ya Kanisa, kutokana na kashfa mbali mbali ambazo zimejitokeza mjini Vatican na Roma katika ujumla wake. Kung’atuka kwa Meya wa Jiji la Roma ni suala la kisiasa ambalo haliusiani kabisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, Baba Mtakatifu alikuwa anazungumzia kashfa zenye mwelekeo wa Kikanisa, kwani wanaohudhuria Katekesi zake ni watu wa kawaida ambao mara nyingi wanakwazwa na kashfa zinazotundikwa kwenye vyombo vya habari. Kumbe, Baba Mtakatifu anatambua dhamana na wajibu wa Kanisa, ndiyo maana ameomba msamaha kwa watu kama hawa.

Akichangia mawazo yake, Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales anasema kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya tafakari zinazotolewa kwenye Makundi madogo madogo na vikao vya kawaida vya Mababa wa Sinodi na kwamba, hapa Mababa wa Sinodi wameonesha kipaji cha ugunduzi kinachojikita katika nguvu mpya. Hii ni tafakari kuhusiana na mbinu mpya ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia.

Hati ya mwisho ya Mababa wa Sinodi, inatarajia kujumuisha mapendekezo yaliyotolewa kwenye Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia, iliyoadhimishwa mwaka 2014 pamoja na mapendekezo yatakayotolewa na Mababa wa Sinodi kwa wakati huu. Hati ya kutendea kazi ya wakati huu inahitaji bado kufanyiwa marekebisho, ili kupata mwelekeo wa nguvu utakaoliongoza Kanisa katika tafakari zake za kitaalimungu.

Kardinali Rùben Salazar Gòmez, Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM, anasema kwa sasa Mababa wa Sinodi wanaendelea kuchangia mawazo katika hati itakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu kama mapendekezo kutoka kwa Mababa wa Sinodi, ambayo yanaweza kufanyiwa kazi na Baba Mtakatifu wakati wa kuandika Waraka wa kitume mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia.

Lengo ni kujenga matumaini kwa wanandoa na familia ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Kanisa kwa wakati huu linaendelea kusikiliza sauti za wanafamilia, hususan wale ambao wanaishi katika hali ngumu ya maisha, ili waweze kupewa msaada wanaohitaji. Mababa wa Sinodi wanaongozwa na uzuri na utakatifu wa Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa na familia. Mafundisho haya ni jibu muafaka kwa changamoto na shida mbali mbali zinazojitokeza katika utume wa ndoa na familia.

Kwa upande wake, Kardinali Philippe Ouèdraogo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ouagadougou, Burkina Faso, anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya makundi madogo madogo yanataka kukazia mwelekeo wa Ulaya kuhusiana na masuala ya ndoa na hivyo kusahau matatizo na changamoto zinazojitokeza sehemu nyingine za Kanisa kama vile Bara la Afrika kuhusiana na ndoa za wake wengi; changamoto kubwa na endelevu Barani Afrika.

Hapa Mababa wa Sinodi wanakumbushwa umuhimu wa kuzingatia tamaduni na asili ya watu. Injili itaweza kueleweka zaidi ikiwa kama waamini watakuwa na ujasiri wa kubadili mawazo yao kama ambavyo Mtakatifu Yohane wa XXIII alivyokaza kusema. Hii inatokana na ukweli kwamba, bado kuna nchi ambazo ziko kwenye Uinjilishaji wa awali, kumbe ni wajibu wa Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, wanawasaidia Watu wa Mungu kufahamu mpango wa Mungu katika maisha ya ndoa na familia.

Mababa wa Sinodi kutoka Afrika wamekuja si kwa ajili ya kukumbatia tamaduni za watu wengine, bali kwa pamoja kumtafakari Kristo Yesu, msingi wa Injili pamoja na kuangalia changamoto za wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo bila kusahau changamoto na kinzani katika kazi ya Uumbaji na Familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.