2015-10-15 14:59:00

Sera na mikakati ya kiuchumi izingatie mahitaji ya watu mahalia na maadili


Mikakati ya maendeleo ya kiuchumi katika maeneo mahalia inaonekana kuwa ni jibu muafaka katika kukabiliana na changamoto za utandawazi wa kiuchumi katika ulimwengu mamboleo; wakati mwingine matokeo yake yana madhara makubwa kwa maisha ya watu. Uchumi mahalia ni chachu, dira na mwelekeo sahihi katika utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo Kimataifa kwa mwaka 2030. Hapa wananchi hawana budi kusimama kidete, kulinda mazingira sanjari na kujikita katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Hii ni sehemu ya ujumbe ambao Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia Bwana Piero Fassino, Meya wa Mji wa Torino kama sehemu ya maadhimisho ya Kongamano la kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya maeneo mahalia, lililofunguliwa tarehe 13 na linatarajiwa kuhitimishwa tarehe 16 Oktoba 2015. Utekelezaji wa ajenda za maendeleo kwa ifikapo mwaka 2030 ni muhimu sana, lakini kwa bahati mbaya, matokeo ya mikakati hii mara nyingi hayajioneshi kwa kiasi kikubwa, kwani ni sera ambazo zinalenga kutuliza dhamiri za watu.

Licha ya mikakati hii ya kimataifa, lakini ikumbukwe kwamba, kuna watu halisi na serikali zinazoishi na kupambana na hali mbaya ya kiuchumi na kwamba, zinataka kuwa ni wadau katika mchakato wa kujiletea maendeleo yao. Maendeleo endelevu hayana budi kutoa kipaumbele cha pekee kwa utu na heshima ya binadamu na mshikamano wa dhati unaojikita katika kanuni auni pamoja na kutunza mazingira, nyumba ya wote. Mafungamano ya kijamii ni muhimu sana katika utekelezaji wa sera na mikakati ya kiuchumi.

Katika dira na mwelekeo kama huu, anasema Baba Mtakatifu Francisko sera za uchumi mahalia ni muhimu sana katika kukabiliana na utandawazi wa kiuchumi ambao wakati mwingine umekuwa ni chimbuko la magumu na machungu kwa watu wengi duniani. Wakati akizungumza na Baraza la Umoja wa Mataifa, wakati wa hija yake ya kitume kwenye Umoja wa Mataifa, Baba Mtakatifu alionesha njia rahisi kabisa ya kuweza kutekeleza ajenda ya maendeleo kimataifa kwa mwaka 2030 kwa kujikita katika maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuwawezesha watu kuwa na makazi bora na salama; ajira na ujira sahihi; chakula bora na cha kutosha; maji safi na salama; uhuru wa kidini na uhuru wa mtu katika masuala ya elimu.

Yote haya yanaweza kupata mafanikio makubwa, ikiwa kama yatafanyiwa kazi katika ngazi ya maeneo mahalia. Kwa ufupi, mikakati na sera za maendeleo endelevu inaweza kutekelezwa katika maeneo madogo madogo ambayo yanaweza kuonesha ufanisi mkubwa. Athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni matokeo ya mfumo wa uchumi unaotaka maendeleo ya wengi, kwa kuwatambukiza watu katika ulaji wa kupindukia, huku makampuni na wafanyabiashara wakitafuta faida kubwa kwa gharama ya maskini na wanyonge; kielelezo cha kumong’onyoka kwa maadili na utu wema; mambo yasiyozingatia haki na mafao ya wengi.

Wanasiasa na wachumi wanapaswa kuhakikisha kwamba, sera na mikakati yao inafumbata na kuambata kanuni maadili, ili kuweza kufanikisha maamuzi yao. Wajumbe wa jukwaa la maendeleo ya watu mahalia waendelee kuhimiza kanuni maadili kwa kukataa katu katu uchu wa faida kubwa ambao umepelekea athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Mikakati ya kiuchumi ilenge mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.