2015-10-15 11:00:00

Mh. Padre George Desmond Tambala, O.C.D. ateuliwa kuwa Askofu wa Zomba, Malawi


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Padre George Desmond Tambala, O.C.D kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Zomba, Malawi. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule alikuwa ni mshauri wa Shirika la Wakarmeli, Makao makuu, mjini Roma. Askofu mteule alizaliwa kunako tarehe 11 Novemba 1968, Jimbo Zomba. Baada ya masomo na majiundo ya Kitawa huko Enugu, Nigeria na Tangaza, Nairobi, akaweka nadhiri zake za daima tarehe 15 Agosti 1995 na kupadrishwa tarehe 13 Aprili 1996.Tangu wakati huo ametekeleza dhamana mbali mbali katika maisha y ana utume wa Kanisa kama Paroko msaidizi,Parokia ya Kapiri Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi kati ya mwaka 1996 hadi mwaka 1998. Mwaka 1998 hadi mwaka 2000 alikuwa masomoni Hispania.

Baadaye akateuliwa kuwa ni mlezi wa Watakaji Kanda ya Wakarmeli, nchini Malawi utume alioutekeleza kati ya mwaka 2000 hadi mwaka 2002. Kunako mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika na Mwakilishi wa Shirika Kanda ya Malawi na Mkurugenzi msaidizi wa Kituo cha Tasaufi cha Mtakatifu Yohane wa Msalaba, Nyungwe- Blantyre, Malawi.Kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2015 akachaguliwa kuwa mshauri wa Shirika la Wakarmelitani,  kwa ajili ya Afrika na Madagascar. Mwaka 2015 amekuwa ni mshauri mkuu wa Navarra, Malawi na Rais wa Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Malawi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.