2015-10-14 14:51:00

Watanzania wanaomboleza kifo cha Waziri Kigoda! RIP.


Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Abdallah Omari Kigoda ambaye aliaga dunia, Jumatatu, Oktoba 12, 2015 katika Hospitali ya Apollo mjini New Delhi, India, ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu tokea Septemba 19, mwaka huu. Alikuwa na umri wa miaka 62.

Katika salamu za rambirambi ambazo amemtumia Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter Kayanza Pinda, Rais Kikwete amesema: “Kwa hakika, nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za kifo cha Waziri Kigoda ambacho nimetaarifiwa kuwa kimetokea India ambako alikuwa anapata matibabu tokea mwezi uliopita.”

Ameongeza Rais Kikwete katika salamu zake hizo za rambirambi: “Kama unavyojua, namfahamu vizuri Mheshimiwa Kigoda. Alikuwa Waziri wangu. Nimefanya kazi naye kwa karibu na kwa miaka mingi ndani ya Serikali yetu. Alikuwa mtumishi hodari, mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa wananchi wa Tanzania, na hasa wananchi wa Jimbo la Handeni, ambao aliwawakilisha kwa miaka mingi akiwa Mbunge wao. Tutakosa utumishi wake mahiri sana.” “Nakutumia wewe Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu wa nchi yetu salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Kigoda. Aidha, kupitia kwako namtumia rambirambi nyingi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna Semamba Makinda na Wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Nakuomba pia unifikishe salamu zangu za rambirambi kwa wananchi wa Jimbo na Wilaya ya Handeni ambao wamepoteza Mbunge wao aliyewatumikia kwa ustadi mkubwa kwa miaka mingi. Aliwawakilisha vizuri na kujali sana maslahi yao.“ Amesisitiza Rais Kikwete: “Kupitia kwako, Waziri Mkuu pia naitumia familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Mheshimiwa Kigoda kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki yao mpenzi. Yajulishe makundi yote hayo kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa, uchungu wao ni uchungu wangu na majonzi yao ni majonzi yangu. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu ya uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi. Pia naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Dkt. Abdallah Omari Kigoda”. Amen.

Kutoka Ikulu, Dar es Salaam.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.