2015-10-14 10:54:00

Uhuru wa kidini, usalama na maendeleo Barani Ulaya!


Haki msingi za binadamu ni dhana iliyoibuka Barani Ulaya kunako karne ya kumi na nane na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakaivalia njuga na kuipatia mwelekeo wa pekee katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni sanjari na mahusiano na Serikali mbali duniani, lengo likiwa ni kudumisha uhuru wa kidini, usalama na kushiriki katika mchakato wa maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili. Uhuru wa kidini ni msingi wa uhuru wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, kwani unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia.

Papa Francisko anaendelea kukazia kwamba, uhuru wa kidini ni msingi wa maendeleo ya wengi na mafungamano ya kijamii. Kutokana na umuhimu wake, Vatican imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha uhuru wa kidini katika medani za Jumuiya ya Kimataifa, kwa kukemea vikali misimamo mikali ya kidini ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa kwa watu wasiokuwa na hatia sanjari na kuvuruga mchakato wa demokrasia ya kweli. Kanisa lina haki ya kushiriki katika maisha ya hadhara kwani linapania kumhudumia mwanadamu mzima: kiroho na kimwili, daima likijitahidi kutafuta mafao ya wengi.

Huu ni mchango ambao umetolewa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, Jumanne, tarehe 13 Oktoba 2015 alipokuwa anachangia mada kwenye mkutano wa mwaka wa Taasisi ya maendeleo na uchumi kimataifa, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Uhuru wa kidini, usalama na maendeleo Barani Ulaya”. Mkutano huu umehudhuriwa pia na viongozi wa ngazi ya juu kutoka Serikali ya Italia.

Askofu mkuu Gallagher anasema, leo hii kutokana na hofu juu ya uhuru wa kidini Barani Ulaya, imekuwa ni vigumu sana kwa waamini kutolea ushuhuda wa imani yao katika maisha ya hadhara, kwani wanaweza kujikuta wakibaguliwa na kutengwa kwa misingi ya kidini. Anakumbusha kwamba, Wakristo Barani Ulaya wanatengwa na kubaguliwa sana ikilinganishwa na waamini wa dini nyingine; mwelekeo unaoenea sana hata katika sehemu nyingine za dunia.

Changamoto hii imepelekea Baraza la Ulaya kuanzisha mbinu mkakati wa kupambana na sera za ubaguzi wa kidini hususan dhidi ya wakristo, kwa kujenga utamaduni wa watu kuishi kwa amani na utulivu; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, kila mtu akijitahidi kuchangia katika ujenzi na ustawi wa nchi yake. Hii ni changamoto pia kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanatoa malezi na majiundo makini kwa watoto wao mintarafu imani yao bila kubaguliwa wala kunyanyaswa. Jamii inapaswa pia kuwa na makini na waamini wenye misimamo mikali, kwani wanaweza kuwa ni chanzo cha maafa na kinzani za kijamii.

Shirikisho la Usalama na Maendeleo Barani Ulaya, OSCE, katika kipindi cha miaka arobaini tangu kuanzishwa kwake, limetoa kipaumbele cha kwanza kwa uhuru wa kidini kama sehemu ya sera na mikakati yake ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu na demokrasia. Lakini hadi sasa kuna kinzani na migogoro inayojitokeza katika majadiliano ya kidini. Ikumbukwe kwamba, dini zina mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya watu, ikiwa kama kutakuwepo na majadiliano ya kidini yanayojikita katika: ukweli, uwazi, heshima na mafao ya wengi.

Askofu mkuu Gallagher anakaza kusema, uhuru wa kidini unapaswa kuwa kwa wananchi wote na wala si kwa baadhi ya makundi ya waamini, kwa kukazia sheria na kanuni, ndiyo maana Kanisa linakazia uhuru wa kidini kuwa ni msingi wa haki zote za binadamu. Misimamo mikali ya kidini ni adui mkubwa wa uhuru wa kidini na kamwe haitoi heshima kwa binadamu. Kumbe, majadiliano ya kidini hayana budi kuendelezwa kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi; usalama na maendeleo ya Bara la Ulaya. Kuna haja ya kuondokana na woga usiokuwa na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.