2015-10-14 15:41:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa


Tunakuleteeni habari njema ya furaha tunapotafakari pamoja ujumbe wa Neno aliyefanyika mwili, Mfalme wa mbingu na nchi. Ni Dominika ya 29 ya mwaka B, Neno la Mungu latualika kuwa watumishi badala ya kutumikiwa, kuwatanguliza wengine badala ya kutangulia sisi, ndiyo kusema kuwa na moyo wa mapendo kwa taifa la Mungu, kuwa na mapendo ya kichungaji.

Mpendwa msikilizaji kipindi tafakari, katika dunia hii watu hupenda kuwa na madaraka, vyeo mbalimbali, kushinda vita, kufaulu mitihani na mambo kama hayo! Lakini leo tunapotafakari Neno la Mungu tunaona jinsi Mungu anavyotualika kuwa na mtizamo tofauti na mtizamo wa ulimwengu. Nabii Isaya katika somo la I toka sura ya 53 anatuwekea sura ya mtumishi aliyechubuliwa uso na kuhuzunika. Jambo hili latupa changamoto kubwa mno, yaani mkristu ni kutumika na si kutumikiwa. Mfano kamili wa jambo hili ni Yesu Kristu mjumbe wa Agano Jipya anayejitoa maisha yake kwa ajili ya wengine pasipo kujibakiza.

Nabii Isaya akitafakari mateso ya Bwana na jinsi gani anavyojitoa maisha yake yote, haachi kuona matunda ya kazi hiyo ya Masiha. Kwa njia ya Nabii Isaya Mungu anasema, kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki, naye atayachukua maovu yao yote.

Mpendwa mwana wa Mungu, kazi ya kutokomboa imetokana na mapendo ya Bwana kwetu sisi kwa njia ya msalaba, na hivi mwaliko kwetu ni huo, kujitoa na kutumikia kwa ajili ya kuleta amani na upendo katika Jumuiya zetu, hata tukidaiwa sadaka kubwa, kama tusomavyo katika kituo cha kumi cha njia ya Msalaba. Katika Somo la pili kutoka katika Barua kwa Waebrania, mtumishi mwaminifu tuliye msikia katikia somo la kwanza ni yule ambaye anachukua mwili wa mtumwa ili afahamu vema shida za mwanadamu aliyeingia katika hali ya utumwa kwa sababu ya kiburi chake na kwa jinsi hiyo mtumishi huyu mwaminifu aweze kutujalia mwili mtukufu utakaofufuliwa siku ya mwisho. Kuchukua mwili wetu maana yake anataka kukaa nasi na kushiriki shida zetu, ndiyo namna ya kutupenda na kutuinua toka katika dhambi zetu. Kuhani huyu pamoja na kushiriki ubinadamu wetu jambo moja tu hakushiriki, nalo ni lile la kutenda dhambi.

Mpendwa mwana wa Kanisa, katika somo la Injili Mitume wanaonesha udhaifu mkubwa juu ya madaraka, bado hawajaelewa vema nini kazi ya Masiha, wanafikiri kuwa Masiha ni kwa ajili ya mamlaka ya kisiasa na kwa masilahi binafsi! na kwa namna hiyo wanadai vyeo vya kisiasa badala ya vyeo vya kitume yaani kuchunga taifa la Mungu kwa kutumika na kutumikia. Bwana akijua udhaifu huo anawakemea kwa nguvu na kuwambia kuwa, mwenye kutaka mamlaka lazima awe mtumishi wa wote.

Ndugu yangu mpendwa, kemeo la Bwana na mafundisho yake si kwa ajili ya Mitume tu bali kwa mataifa na vizazi vyote, na hivi anatuambia sisi leo, yakuwa uongozi ni kutekeleza mapenzi ya Mungu, yaani kujitoa kiaminifu kama Kristu alivyojitoa kufa msalabani kwa ajili ya wengine. Uongozi si kudai heshima wala upendeleo ambavyo hutengeneza matabaka bali ni mshikamano na Kristu mtumishi mwaminifu.

Mpendwa ninazidi kukualika kutafakari vema tendo la kutumikia na hasa katika mwaka huu ambapo tunaalikwa kujikita zaidi katika kuelewa vema juu ya karama ya huruma na msamaha nyenzo zinazoboresha imani yetu, imani iliyotendaji, imani inayodai matendo thabiti yaliyo ya wazi na ushuhuda wa kimisionari. Basi nikuombee baraka tele za Mungu ili uzidi kuimarika katika utumishi na huruma kwa wengine alama ya mapendo makamilifu kwa Mungu na kwa jirani. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.