2015-10-14 11:54:00

Lindeni watoto na familia, ili kuonesha uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza katekesi yake juu ya Familia, kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano tarehe 14 Oktoba 2015 amewatembelea na kusalimiana na wagonjwa waliokuwa wanafuatilia Katekesi yake kwenye Ukumbi wa Paulo VI, kwa kuhofia mvua! Baba Mtakatifu amesalimiana na baadhi yao na kisha kuwapatia baraka yake ya kitume! Baba Mtakatifu kwa niaba ya Kanisa ameomba msamaha kutoka na kashfa ambazo zimejitokeza hivi karibuni mjini Vatican na kwa mji wa Roma ambazo zimepeleka Mstahiki meya kuachia ngazi ya madaraka!

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee wakati wa katekesi yake amejikita katika ahadi ambazo wazazi wanawapatia watoto wao wanapozaliwa hapa duniani. Kati ya ahadi hizi ni upendo thabiti na kwamba, kila mtoto anatumaini kwamba, atapendwa na kutunzwa. Ahadi hii inapovunjika matokeo yake ni “Kashfa” ambayo Yesu anasema “Angalieni msidharau mmojawapo wa wadogo hawa, kwa maana nawambia ya kwamba Malaika zao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni”. Mt. 18: 10.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa katika maadhimisho ya Sakramenti ya Ubatizo linatoa ahadi kwa watoto wake wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu. Hizi ni ahadi ambazo zinapaswa kulindwa na kutunzwa na wazazi, wasimamizi wa ubatizo na Jumuiya yote ya Wakristo! Kwa kufanya mang’amuzi na uzoefu wa upendo, kila mtoto anatambua na kuonja uwepo wa Mungu anayewapenda watoto. Hili ni jambo muhimu sana kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha mahusiano haya ya Kimungu kwa kutoa nafasi ya Mungu katika maisha ya watoto wadogo.

Wazazi kwa njia pamoja na mapendo ya dhati kwa watoto wao, yanawasaidia kuheshimu utambulisho na upekee wao kama watoto wa Mungu. Yesu anawafundisha wafuasi wake kuwa kama watoto wadogo kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu; kwa kuwalinda watoto na familia kama kielelezo cha kutunza ahadi kubwa ya Mungu ambayo amewakirimia kwa njia ya watoto hawa na kwa ajili ya familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa mahujaji na wageni kutoka DRC. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia ni fursa kwa Kanisa kusali kwa ajili ya kuombea familia, lakini zaidi watoto wadogo, ili waweze kuibua na kukuza upendo kwa Mungu na jirani zao. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kuendelea kuombea Sinodi ya Maaskofu, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu duniani kwa njia ya maisha ya kifamilia.

Familia ya Mungu iendelee kuwasaidia wazazi ili kuwahakikishia watoto wao maisha mema na imani tele, daima wakiwaombea wazazi kutambua na kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha. Waamini wawaombee Mababa wa Sinodi ili waweze kuchukua mawazo mema yanayojitokeza katika maadhimisho ya Sinodi ya Familia.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka Mwenyeheri Honorat Kozminski, mwamini aliyekuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, ambaye masalia ya mwili wake yataoneshwa hadharani huko mjini Varsavia, Poland. Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani na Novena ya maandalizi ya Maadhimisho ya miaka mia moja tangu alipofariki dunia, Baba Mtakatifu anawaalika watawa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia moyo wa uaminifu na miito mitakatifu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini katika Mwezi huu wa Oktoba kuunga mkono juhudi za kimissionari zinazotekelezwa na Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, kwa kusali na kuonesha mshikamano wa dhati; vijana wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu na wagonjwa sadaka na majitoleo yao ni muhimu kwa wale ambao bado hawajamtambua Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 17 Oktoba 2015 ni Siku ya Kimataifa ya kupambana na Umaskini. Lengo ni kuongeza nguvu katika kukabiliana na umaskini  na ubaguzi, ili kuhimiza umuhimu wa kuzingatia haki msingi za binadamu. Waamini wote wanahimizwa kutekeleza nia hii njema, ili upendo wa Kristo uweze kuwafikia na kuwafariji maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.