2015-10-14 11:28:00

Elimu: huduma kwa maskini na kuendeleza mchakato wa upatanisho!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI limegharimia ujenzi wa shule ya Sekondari mjini Kinshasa, ambayo imepewa jina kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko, kama kielelezo cha mshikamano na watu wanaoteseka kutokana na majanga mbali mbali ya maisha. Ni mwaliko wa kutoka ili kuwaendea wale ambao wamesukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa.

Shule hii itaweza kutoa huduma ya elimu kwa wanafunzi mia sita wa Sekondari wenye umri kati ya miaka kumi hadi kumi na sita. Shule inasimamiwa na kuendeshwa na Shirika la Watawa wa Mabinti wa Mateso ya Yesu Kristo na Bikira Maria mwenye huzuni. Lengo ni kuendeleza huduma kwa maskini; kujenga na kuimarisha mchakato wa umoja na upatanisho wa kitaifa pamoja na kupambana na janga la ujinga na umaskini.

Uzinduzi wa shule hii umefanywa hivi karibuni kuwa kuwahusisha viongozi wa Kanisa na Serikali na kwamba,  Monsinyo Timothèè Bodika Masinyai, alimwakilisha Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC. Mradi huu umefadhiliwa pia na Shirika Lisilo la Kiserikali la “Semi di Pace” kutoka Italia ambalo linakazia umuhimu wa elimu kama ufunguo wa maendeleo ya jamii. Kwa bahati mbaya, elimu nchini DRC imekuwa ni haki kwa watoto wachache kutokana na vita, kinzani na chokochoko zinazoendelea nchini humo kiasi cha kuvugura misingi ya haki na amani, mambo msingi katika kukuza utulivu na maendeleo.

Elimu inapania kuwajengea uwezo vijana wa DRC ili kuweza kupambana na changamoto za maisha na hatimaye, kuondokana na ndoto za kupata mafanikio na utajiri wa haraka haraka kwa kujiunga na makundi ya kijeshi au biashara ya ukahaba na ngono barabarani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.