2015-10-13 09:42:00

Waonjesheni vijana mshikamano na imani thabiti ili kukabiliana na changamoto!


Kutokana na mtikisiko wa uchumi kimataifa, vijana wengi wanajikuta wakiwa wamekata tamaa kutokana na kukoswa fursa za ajira, Jumuiya ya Kikristo kwa namna ya pekee, inahamasishwa kuhakikisha kwamba, inawaonesha vijana hawa mshikamano wa dhati na imani katika hija ya maisha yao, ili wasikate tamaa, tayari kusimama kidete kujenga na kudumisha maisha ya kiutu yanayojikita katika msingi thabiti wa Yesu Kristo.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa Familia ya Mungu Jimboni Molise, Kusini mwa Italia, kama kumbu kumbu ya mwaka mmoja, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Jimboni humo, kunako tarehe 5 Julai 2014. Wakati huo, Baba Mtakatifu alibahatika kukutana na bahari ya vijana, kiasi cha kuonja maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, chemchemi ya imani na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya.

Vijana hawana budi kutoka katika mzunguko wa kukata tamaa, kwa kuonjeshwa ujasiri, mshikamano na imani; tayari kuwasindikiza katika mchakato wa kutambua na kuthamini utu na heshima yao. Wasichana ni waathirika wakuu katika ulimwengu wa ajira anasema Kardinali Parolin, lakini wakisimama kidete kulinda na kutetea utu wao, wanaweza kupata mafanikio makubwa kama inavyoshuhudiwa na wasichana wa shoka kutoka katika eneo hili ambao waliyakita maisha yao katika ufugaji, leo hii ni mfano bora wa kuigwa na wengi.

Huu ndio wito ambao vijana wanapaswa kushirikishwa kwa umakini mkubwa, ili kweli waweze kuwa ni watunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote, kama anavyo kaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Vijana wajifunze kudumisha maisha ya sala, sadaka, majitoleo pamoja na kushirikiana na wengine.

Kardinali Parolin katika mahubiri kwenye Ibada ya Misa Takatifu aliyoadhimisha kwenye Kanisa kuu la Campobasso na kuhudhuria na Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini, amegusia hali ya vijana wengi wanaotafuta maana ya maisha, lakini kwa bahati mbaya wanajikuta wakitumbia katika njia za mkato na hivyo kubaki wakiwa wanaelea katika upweke na utupu! Vijana wanakumbushwa kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini ya kweli na kamwe hawezi kuwadanganya.

Vijana wajifunze kuwa na busara ili kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha. Busara ni chemchemi inayomkirimia mtu amani ya kweli, utulivu na furaha ya kweli. Busara ni fadhila inayoweza kupatikana kwa wote bila ubaguzi, jambo la msingi ni mwamini kuonesha moyo wa unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kusikiliza kwa makini, tayari kumfuasa Yesu ambaye ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha hekima ya Mungu.

Vijana wawe tayari kujitisa kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani na kamwe wasiwe na moyo mgumu kama yule kijana tajiri anayezungumziwa kwenye Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 28 ya Kipindi cha mwaka B wa Kanisa. Vijana wawe na ujasiri wa kujenga na kudumisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao pasi na papala katika maisha. Kwa kumwaminia na kujiaminisha kwa Yesu, vijana wanaweza kuwa na busara katika safari ya maisha yao ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.