2015-10-13 09:31:00

Utunzaji bora wa mazingira utoe kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya binadamu!


Mkutano wa kimataifa juu ya watu, mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa maisha ya binadamu, umehimitishwa, Jumatatu, tarehe 12 Oktoba huko Cochabamba, nchini Bolivia. Ni mkutano ambao ulifunguliwa rasmi, Jumamosi tarehe 10 Oktoba 2015, kwa lengo la kuibua mbinu mkakati wa utunzaji bora wa mazingira, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya binadamu.

Katika ujumbe uliotumwa kwa washiriki wa mkutano huu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahimiza kufuata mchakato wa ekolojia ya haki, kwa ajili ya maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu. Mkutano huu wa kimataifa umehitishwa na Rais Evo Morales, Rais wa Bolivia, ili kusikiliza mchango unaotolewa na vyama vya kijamii katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Wajumbe wamehimizwa kujikita katika maendeleo endelevu yanayojikita katika haki jamii, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi na mafao ya wengi. Maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huo wa mabadiliko ya tabianchi kimataifa, yatawasilishwa kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-Moon kama sehemu ya mchango wao katika mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi (Cop21) unaotarajiwa kufanyika Paris, nchini Ufaransa, Mwezi Desemba, 2015. Zaidi ya wajumbe elfu sita kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameshiriki. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa naye pia alikuwa amealikwa ili kutoa ujumbe kwa washiriki hawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.